Breaking News

Prof Mbarawa Akemea Vitendo Vya Rushwa Katika Miradi.

Related image
DAR ES SALAAM:
Waziri wa Ujenzi,Uchukuzi na Mawasiliano Profesa MAKAME MBARAWA ameiagiza bodi ya usajili wa wabunifu majengo na wakadiriaji wa majenzi kuwafutia usajili na kuwachukulia hatua kali wataalam wote watakaobainika kupokea au kutoa rushwa katika kutekeleza wajibu wao.

Akizungumza jijini Dar es salaam katika ufunguzi wa mkutano wa 28 wa wadau wa bodi ya usajili wa wabunifu majengo na wakadiriaji wa majenzi  amesema kuwa ni muhimu kwa bodi kufanya ukaguzi wa mara kwa mara katika miradi ili kubaini wale wote wanaukiuka taratibu kwaajili ya rushwa.

Waziri MBARAWA ameipongeza bodi hiyo kukutanisha wataalam hao  na wadau wa bodi ya nchini Kenya na kuwataka kuendelea kukutana kubadilishana ujuzi na uzoefu kwakuwa teknolojia inakua kwa kasi sana hivyo ni vema kujifunza zaidi ili kukabiliana na majanga kama matetemeko ya ardhi.

Pia ameipongeza bodi hiyo kwa kubuni michoro  ya majengo kwa gharama nafuu na kusema kuwa itawanufaisha  watanzania katika kutatua matatizo ya ujenzi.

Aidha Profesa MBARAWA ametoa agizo kwa wakurugenzi na watendaji wa masuala yanayohusu ujenzi kuhakikisha vijana wanapewa fursa ya kuwekwa katika kila sehemu yenye miradi mkubwa  ili waweze kujifunza na kunufaika kupitia miradi hiyo.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa bodi ya usajili wa wabunifu majengo na wakadiriaji majenzi ALBERT MUNUO amesema kuwa semina hiyo ni mwendelezo wa mpango wa mafunzo endelevu ambazo bodi imekuwa  ikiandaa kwa lengo la  kuwakutanisha wabunifu wa majengo,wakadiriaji majenzi na wataalam wanaohusiana na sekta ya ujenzi lengo likiwa kujifunza mambo mapya yanayotokea katika utendaji kazi.

Mkutano huo wa bodi  umewakutanisha wadau na wataalamu wa majenzi na makandarasi mada kuu ni mbinu ya kupunguza madhara ya matetemeko ya ardhi,ukaguzi wa miradi ya ujenzi na matengenezo ya majengo na miundombinu.

No comments