Dk. Shein Afunguwa Maonesho Siku Ya Chakula Duniani Zanzibar
Na waziri yakoub
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.
Ali Mohamed Shein amesema kuwa katika kipindi cha hivi karibuni dhamira njema
ya kuwapa eka tatu wananchi kwa ajili ya kilimo iliyooneshwa na uongozi wa
Serikali tangu awamu ya Kwanza hadi hii ya Saba, imeanza kuharibiwa na baadhi
ya wananchi kwa kuziuza eka hizo na wengine kuzikata viwanja vya kujenga nyumba
na kuwauzia watu.
Dk. Shein aliyasema hayo leo katika ufunguzi wa maonesho ya Siku ya Chakula Duniani,
yaliofanyika huko Kizimbani na kuhudhuriwa na wananchi pamoja na viongozi mbali
mbali akiwemo Makamo wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Idd, Mama Mwanamwema Shein
na viongozi wengine wa vyama vya siasa na Serikali.
Katika hotuba yake, Rais Dk. Shein alisema kuwa kitendo
hicho si kizuri kwani kinavunja mwelekeo wa azma ya Mapinduzi matukufu ya
Januari 12, 1964 sambamba na kupelekea vizazi vijavyo kukosa sehemu za kilimo
na hatimae kuagiza vyakula nje ya nchi.
Aliongeza kuwa ipo haja ya kuzingatia matumizi mazuri ya
ardhi ndogo iliyopo kwa kutenga maeneo ya kilimo, maeneo ya makaazi na shughuli
nyengine za kiuchumi sambamba na kuzingatia sheria za Mipango Miji na Vijiji.
Aliongeza kuwa hivi sasa Zanzibar ina watu milioni 1.4
hali hiyo inachangia kuwa na matrumizi makubwa ya ardhi hasa kwa ajili ya
makazi na kupnguza ardhi ya kilimo, hivyo wananchi wanapotaka kujenga ni vyema
wakapeka maombi yao katika Wizara ya Ardhi, Maji, Nishati na Mazingira ili
waelekezwe taratibu ziliopo.
Alisema kuwa hivi sasa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
imeamua kufanya Mapinduzi ya Kilimo kwa kukifanya kilimo kuwa cha kisasa na cha
kitaalamu hatua ambayo imeanza kuzaa matunda kwa kuongezeka kwa kiwango cha
mavuno na mazao mbali mbali hasa mazao ya chakula yanayolimwa hapa nchini.
No comments