Cuf Ya Lipumba Yaikana Cuf ya Maalim.
Chama cha Wananchi(CUF), upande wa
Profesa Ibrahim Lipumba kimesema kitashiriki kikamilifu katika uchaguzi
wa madiwani uliopangwa kufanyika Novemba 26 lakini kimesisitiza kutoshirikiana
na Ukawa.
Hii ni mara ya kwanza kwa chama hicho
kuweka msimamo wake katika uchaguzi tangu kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka
2015 ambapo CUF ilikuwa miongoni mwa vyama viliunda umoja huo kwa kuweka
wagombea waliokubaliana.
Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa
CUF, Abdul Kambaya amesema jana Jumamosi jijini kuwa chama hicho hakioni
sababu yoyote ya kushirikiana na vyama vingine kwenye uchaguzi huo ambao
unahusisha halmashauri 34.
“CUF tunashiriki kwenye uchaguzi huu
lakini hatututegemei kushirikiana na umoja wowote ule, sisi hatuitambui Ukawa
lakini tunajua kuna chama kama Chadema, CUF na vyama vingine,” alisema Kambaya
wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za chama hicho
zilizopo Buguruni.
Alisema chama hicho kimejipanga
vilivyo kuelekea kwenye uchaguzi huo na kwamba ili kuwaletea maendeleo wananchi
wa maeneo hayo kunahitajika kuwa na viongozi wenye utulivu wa akili.
“Sisi tuko tayari kuelekea kwenye
uchaguzi huo bila kuhusishwa na chama kingine chochote tunaamini tutafanya
vizuri,” alisema.
Awali, mkurugenzi wa uchaguzi wa
chama hicho, Jafari Mneko aliwataka wana CUF kujitokeza kwa wingi katika
kinyang’anyiro hicho. Amesema chama chake kimepokea taarifa kutoka ofisi ya
Tume ya Taifa ya Uchaguzi ikiwaarifu kuhusu uchaguzi huo.
“Tumepata barua kutoka tume ambayo
imetueleza kuhusu tarehe ya kufanyika kwa uchaguzi huo na sisi tumeanza
kujiandaa na ndiyo maana tunawaomba wanachama wetu wanaohisi wana uwezo
wajitokeze kuomba nafasi na baadaye viongozi wa chama watachuja majina yao,” alisema.
Katika hatua nyingine mkurugenzi huyo
alionya kile alichokiita mali ya chama kutumika kinyume na sheria na akawataka
wanachama kutetea maslahi ya chama chao.
“Kuanzia sasa hatutapenda kuona mali
ya chama kama mihuri, bendera ikiendelea kuchezewa ovyo, tunawataka wanachama
kuzingatia katiba ya chama ibara ya 12 ambayo inamtaka kila mwanachama kulinda
katiba na imani ya chama,” alisema.
No comments