TGNP Mtandao: sera za kumwezesha mwanamke haziendani na mazingira ya kuelekea tanzania ya viwanda na uchumi wa kati
Mwenyekiti wa Bodi ya TGNP Mtandao,Vicensia
Shule akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) leo Ijumaa Septemba
8,2017 katika ukumbi wa TGNP Mtandao.
Dar es salaam.
Imeeelezwa kuwa sera
mbalimbali za kumwezesha mwanamke na kuinua usawa wa kijinsia nchini haziendani
na mazingira ya sasa katika kuelekea Tanzania yenye viwanda na uchumi wa kati.
Mwenyekiti wa Bodi ya
TGNP Mtandao,Vicensia Shule (pichani) akizungumza wakati akitoa taarifa kwa
vyombo vya habari kuhusu masuala mbalimbali yaliyojiri wakati wa siku nne za
Tamasha la Jinsia mwaka 2017 lililofanyika katika viwanja vya TGNP Mtandao
jijini Dar es salaam kuanzia Septemba 5 hadi 8,2017.
Alisema miongoni mwa
masuala yaliyoibuliwa na washiriki wa Tamasha hilo katika siku hizo nne ni
pamoja na sera za kumwezesha mwanamke kutoendana na mazingira ya sasa mfano
mitaala ya elimu iliyopo haiendani na sera ya kuelekea Tanzania yenye viwanda
na uchumi wa kati.
Alisema washiriki wa
tamasha hilo wamependekeza sera zifanyiwe marejeo ili ziendane na muktadha wa
sasa na ziwe na mrengo wa kijinsia.
“Sera hizo pia ziendane
na miongozo na mikakati mbalimbali ya kitaifa na kimataifa kama vile malengo ya
maendeleo endelevu,ajenda ya Afrika 2063,Mkataba wa Jinsia na Maendeleo wa
SADC,Mpango wa Maendeleo wa miaka mitano na mpango wa taifa wa kutokomeza
ukatili wa kijinsia”,alieleza Shule.
Katika hatua nyingine
alisema ni vyema sasa bajeti kuu za serikali za mitaa zikazingatia mahitaji ya
kijinsia kwa makundi yote huku akisisitiza kuwa ziwe za kutekelezeka na
mchakato wa kuandaa bajeti uwe shirikishi na wa uwazi bila kujali tofauti za
kijiografia,rika,hali ya uchumi,jinsi,elimu na hali ya ulemavu.
“Utengwaji wa rasilimali
pia bado ni changamoto hasa katika kukuza na kuendeleza usawa wa kijinsia na
kuwawezesha wanawake,mfano ni asilimia 20 ya wanawake Tanzania wanamiliki
ardhi”, Aliongeza Shule.
Tamasha la Jinsia la 14
mwaka 2017 lililokutanisha washiriki zaidi ya 1500 kutoka ndani na nje ya
Tanzania, limehitishwa leo Septemba 8,2017 baada ya siku nne za
sherehe,tafakuri,mijadala na pongezi.
Mkurugenzi Mtendaji TGNP Mtandao,Lilian Liundi akizungumza ambapo alisema wataendelea kushirikiana serikali pamoja na mashirika mbalimbali yanayojihusisha na masuala ya kijinsia ili kuhakikisha kunakuwepo na mageuzi ya mifumo kandamizi kwa usawa wa kijinsia na maendeleo endelevu.
No comments