Mkojo Wa Wema Sepetu Ulikuwa Na Bangi: Mkemia
![Related image](https://kiss100.s3.amazonaws.com/wp-content/uploads/2017/01/wema.png)
Kesi ya matumizi ya dawa za kulevya aina ya
bangi inayomkabili mrembo Wema Sepetu jana aliendelea kusikilizwa katika
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ambapo shahidi namba moja kwa upande wa
mashtaka alitoa ushahidi wake na kusema kuwa mkojo wa mrembo huyo ulionyesha
kuwa alivuta bangi.
Shahidi huyo, Elias Mulima kutoka Ofisi ya
Mkemia Mkuu wa Serikali akiongozwa na wakili wa serikali Constantine Kakula
aliieleza mahakama hiyo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba namna
alivyompima mtuhumiwa huyo na kubaini kuwa mkojo wake ulikuwa na bangi ambapo
sampuli ya mkojo huo aliipokea Februari 8.
Shahidi alisema baada ya Wema kutoa sampuli ya
mkojo huo ilipelekwa maabara ambapo lengo lilikuwa ni kuchunguza chembechembe
za uwepo wa dawa za kulevya na ndipo walipobaini uwepo wa dawa za kulevya aina
ya bangi. Baada ya kutoa ushahidi huo, Elias alitoa taarifa ya uchunguzi
aliyoiandaa na kuisaini yeye mwenyewe na pia kuthibitishwa na kaimu mkemia mkuu
wa serikali ili itumike kama kielelezo cha ushahidi.
Baada ya hoja hizo, upande wa utetezi unaoongozwa
na Wakili Peter Kibatala aliitaka mahakama kutopokea taarifa hiyo kwa sababu
uchunguzi haukufuata sheria kwani Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Jinai
inataka uchunguzi wa kitabibu kwa mtuhumiwa ambaye yupo chini ya ulinzi lazima
upate kibali cha mahakama.
Aidha alitaka pia mahakama isipokee taarifa
hiyo kwa sababu haikumbatanaishwa na fomu namba DCEA 001.
Akijibu hoja hizo, hakimu aliyekuwa mahakamani
hapo alisema kuwa, fomu yenye namba 001 inatumiwa na Polisi wanaopeleka sampuli
na fomu namba 009 ni taarifa ya mkemia, na kwamba fomu moja haitegemei nyingine
kwa sababu huandaliwa na watu tofauti.
Hakimu pia aliipangua hoja ya Kibatala ya
kibali cha mahakama ambapo alisema sheria haijasema kuwa wakati wote lazima
Polisi waombe kibali hicho cha uchunguzi wa kitabibu, lakini pale ambapo
mtuhumiwa atakuwa hayupo tayari, wanaweza kuomba kibali cha mahakama.
Kutokana na mvutano ulioibuka mahakamani hapo
kuhusu taarifa hiyo ya uchunguzi, mahakama iliomba muda wa kupitia nyaraka hizo
na kesi hiyo ikaahirishwa hadi Agosti 4 mwaka huu.