RAIS MUGABE AUZA NG'OMBE KUSAIDIA MUUNGANO WA AFRIKA
Zimbabwe imeuza
ng'ombe wa thamani ya $1m (£770,000) kwenye mnada na kukabidhi pesa hizo kwa
Wakfu wa Muungano wa Afrika kusaidia kumaliza utamaduni wa kutegemea fedha
kutoka kwa wafadhili wa nje, Rais Robert Mugabe amesema.
Rais huyo amesema
binafsi alitoa ng'ombe 300 kutoka kwa zizi lake, nao raia wengine wa Zimbabwe
wakaongeza ng'ombe wengine kiasi sawa na hicho.
Bw Mugabe
alikabidhi hundi ya $1m kwa AU wakati wa mkutano mkuu wa viongozi wa mataifa
wanachama nchini Ethiopia.
Mchango huo wa
Zimbabwe umetokea kipindi ambacho taifa hilo linakabiliwa na uhaba wa fedha na
chakula.
![](https://ichef-1.bbci.co.uk/news/660/cpsprodpb/072D/production/_96773810_zimbabwe1.jpg)
Mwaka jana, watu
zaidi ya milioni nne nchini humo walihitaji chakula cha msaada baada ya mvua
kutonyesha vyema.
Hata hivyo, mwaka
huu mavuno yamekuwa tele na taifa hilo linatarajiwa kujitosheleza kwa chakula
kwa mara ya kwanza katika miaka mingi.
Upinzani umelaumu
serikali kwa uhaba huo wa chakula, na kusema kwamba sera yake yenye utata ya
kupokonya wazungu mashamba ilichangia kusambaratisha sekta ya kilimo.
Zimbabwe imelazimika
pia kuanza kutumia hati za dhamana baada ya kuishiwa na dola za Marekani, pesa
ambazo hutumiwa kwa biashara nchini humo.
Kiwango cha juu cha
mfumko wa beii kiliilazimu Zimbabwe kuacha kutumia dola yake mwaka 2009.
Waziri wa mambo ya
nje Simbarashe Mumbengegwi amesema ng'ombe hao sana walitolewa na watu
waliofaidi kutokana na mageuzi katika sera ya mashamba nchini humo, kwa mujibu
wa gazeti la serikali la Herald.
Msaada huo ulikuwa
ni "kuimarishwa" kwa ahadi ya Bw Mugabe ya mwaka 2015 kwamba angetoa
ng'ombe 300.
Akiongea katika
mkutano huo, Bw Mugabe alisema mchango huo ni mdogo tu lakini ni ishara muhimu
katika kujaribu kukomesha utegemezi wa Afrika kwa pesa za wafadhili.
"Kama Mwafrika
na mkulima, kutoa ng'ombe ni jambo la kawaida kwangu, ikizingatiwa kwamba bara
letu limebarikiwa na ng'ombe wengi na ng'ombe hutazamwa kama hazina ya
utajiri," Bw Mugabe alisema.
Kwenye tovuti yake,
Wakfu wa AU unasema huwa unaangazia mipango ya vijana na wanawaje, na kuendeleza
usawa wa jinsia.
Wakati wa kipindi
chake kama mwenyekiti wa AU kati ya 2015 na 2016, Bw Mugabe alitetea AU iwe
ikifadhiliwa na Waafrika.
Kwa sasa asilimia
60% ya bajeti ya umoja huo hutoka kwa wafadhili kutoka nje.
Chanzo: BBC
No comments