SERIKALI YASAINI MKATABA KUPANUA NA KUONGEZA KINA CHA BANDARI YA DAR ES SALAAM
Benjamin Sawe-Maelezo
Mamlaka ya Bandari nchini (TPA), imesaini mkataba wa upanuzi na
uongezaji wa kina cha bandari utakaowezesha bandari ya Dar es Salaam kupokea
meli kubwa za mizigo na kushindana na bandari nyingine katika pwani ya bahari
ya hindi.
Upanuzi huo utakaofanywa na kampuni ya China Harbor Construction
ya China utagharimu kiasi cha shilingi bilioni 336 na utadumu kwa miezi 36,
ambapo utahusisha uongezaji wa kina cha lango la bandari na uongezaji wa kina
cha maji kati ya gati namba 0, 1 hadi 7.
Akizungumza katika hafla ya utiaji saini mkataba huo Waziri wa
Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa amesema hatua hiyo
inalenga kuifufua upya bandari ya Dar es Salaam ili ifanye kazi kwa ushindani
na kuhudumia wateja wengi kuliko ilivyo sasa.
“ Kukamilika kwa upanuzi na uongezaji wa kina cha maji katika
gati namba 1 hadi 7 kutoka mita 8 hadi 15 kutawezesha meli kubwa na za kisasa
zenye uwezo wa kubeba hadi makontena elfu kumi na tisa kutia nanga katika
bandari ya Dar es Salaam na kuongeza ufanisi na kukuza uchumi wa Tanzania”,
amesema Prof. Mbarawa.
Aidha Prof. Mbarawa amesisitiza kuwa pamoja na upanuzi wa
bandari ya Dar es Salaam Serikali inaendelea na ujenzi wa miundombinu wezeshi
ya reli na barabara ili kuhakikisha mizigo haikai muda mrefu bandarini.
“Ujenzi wa reli ya kisasa ya Standard Gauge toka Dare s Salaam
hadi Kanda ya Ziwa na Kigoma na ufufuaji wa reli ya Tazara kutawezesha bandari
ya Dar e s Salaam kufanya kazi kwa ufanisi na kuvutia wafanyabiashara wengi
hivyo nawataka wafanyakazi wote wa bandari kufanyakazi kwa bidii na uadilifu”,
amesisitiza Prof. Mbarawa.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa TPA Eng. Deusdedit Kakoko amesema kiasi
cha dola za Marekani milioni 421, kitapatikana kwaajili ya ujenzi huo ambapo
kati ya fedha hizo Benki ya Dunia itatoa mkopo wa masharti nafuu wa dola
milioni 345.
Kukamilika kwa ujenzi huo kutaondoa adha ya baadhi ya meli
kusubiri kwa muda mrefu kupata nafasi ya kutia nanga na kutaongeza hadhi ya
bandari ya Dar es salaam na kuvutia wasafirishaji wengi kutoka ndani na nje ya
nchi.
No comments