LUQMAN MALOTO: RAIS MAGUFULI, LISU NA ZITTO KABWE WOTE NI WAZALENDO:
Ni Rais mzalendo kwa nchi yake.
Ana uchungu sana kuona watu wanatajirika kwa rasilimali za umma.
Ni kiongozi ambaye anataka kuona watu wananufaika kwa jasho
halali na siyo upigaji.
Ni Rais jasiri mno.
Anaweza kuingia kwenye anga ngumu na kuzitikisa. Kujenga nchi
yenye heshima unahitaji kiongozi mkuu mwenye uthubutu kama Magufuli a.k.a John
The Iron 'Chuma'.
Ni Rais ambaye yupo tayari
kuingia kwenye mgogoro wowote wa ama ndani au nje, mradi tu asimamie kile
ambacho anakiamini.
Iwe yupo sahihi au anakosea,
ikiwa yeye anajiona yupo sahihi, Rais Magufuli huwa hapindi. Husimamia
anachokiamini kwa nguvu zote.
Si mnafiki, si mwoga, si wa
nyekundu na njano au nusu kwa nusu, akisema nyekundu, keshokutwa utamkuta na
nyekundu yake. Hana ndimi mbili.
NAMPENDA TUNDU LISSU
Siku zote hutafuta makosa ya
Serikali na kuyaweka wazi. Hata pale ambapo kila mtu huamini Serikali imepatia
na kuishangilia, Lissu akiibuka utampenda tu.
Anafahamu mantiki ya kuwa
mpinzani kwa nchi za Afrika hususan Tanzania. Anatambua kuwa yeye si sehemu ya
watu wanaopaswa kuiimbia mapambio Serikali inapofanya vizuri.
Anajua kuwa uhai
wa upinzani ni makosa ya Serikali na Chama Tawala, kwa hiyo anakosoa tu.
Uzuri wa Lissu ni kwamba hakosoi
ilimradi aonekane anakosoa, isipokuwa hukosoa kwa hoja na vielelezo yakinifu.
Lissu akizungumza, hata kama sauti yake na maneno yake yanakera lakini wewe
sikiliza ujumbe, hutaambulia sifuri.
Ukiona Lissu anafungua kinywa
ujue amejipanga. Japo yapo maeneo mengi huonekana mpiga kelele lakini ukiona
analibebea bango jambo ujue ana hoja za msingi.
Ni faida kubwa kuwa na Lissu
katika nchi hii, maana haogopi kukosoa. Haogopi nafasi ya anayemkosoa.
Katika nchi ambayo watu wengi
wanaogopa kufunua vinywa vyao kumkosoa Mkuu wa Nchi, angalau sauti ya Lissu
itasikika ikikosoa. Akiwa bungeni au nje ya Bunge, msamiati unaoitwa woga,
haumo kichwani kwa Lissu.
Unamhitaji Lissu kumfanya mtawala
asibweteke.
Hata kama mtawala anafanya vizuri, uwepo wa Lissu husaidia kuchokonoa
hata makosa madogo yenye kujificha na kuyaweka wazi. Katika nchi ni hasara
kubwa kukosa watu wa kuikosoa Serikali.
NAMPENDA ZITTO KABWE
Mwanasiasa muungwana na mzalendo
kwa nchi yake. Si mtoa lugha za kushambulia, isipokuwa hujikita katika kujenga
hoja zenye kuifaa nchi.
Ni mpinzani lakini Serikali
inapofanya sawa husifia. Serikali inapokosea husimama na kukosoa bila woga.
Kila jambo linalofanyika kwa
masilahi ya umma hutakosa kauli ya Zitto. Kauli yake inaweza kuwa chanya au
hasi kulingana na mapokeo yake.
Tabia yake ya kuisifu Serikali
inapofanya vizuri na kuikosoa inapofanya vibaya, humfanya wakati mwingine
ajikute anapokea mashambulizi kila upande; kutoka Chama Tawala, vilevile kwa
wapinzani wenzake.
Zipo nyakati Zitto hujikuta
anatofautiana na wapinzani wenzake pale anapoona hawapo sawa. Ndiye mpinzani
anayeongoza kwa kushambuliwa na wapinzani wenzake, wakati huohuo akishambuliwa
na watu wa utawala.
Ni mwanasiasa mwenye maono
makubwa. Hoja zake si za kukosoa tu, isipokuwa hukosoa, husahihisha na
kuelekeza njia ya kufikia jawabu.
Akisimama bungeni huwa hasemi
"Serikali imeshindwa", bali husema " Serikali inatakiwa ifanye
haya ili ifanikiwe", daima hutoa hoja zenye thamani kubwa. Hutoa hoja za
dhahabu. Zitto si mlalamikaji, ni mtoaji wa ufumbuzi kisha husherehesha
ufumbuzi wake.
Wakati mwingine hoja zake na
namna ambavyo huzitoa kwa uchambuzi wa kina, huwafanya watu waone anajifanya
anajua. Kiukweli Zitto ni fundi hasa katika kujenga hoja.
Muogope sana Zitto akizungumzia
jambo baada ya kitambo japo kifupi. Hapo ujue tayari ameshasoma na ameshakuwa
na pointi nyingi kichwani.
Unamhitaji Zitto kwa ajili ya
kupata sura ya pili, maana anapokosoa sura ya kwanza, huja na uchambuzi wa kina
kuhusu faida za sura ya pili. Ndiye kiongozi mwenye hoja mbadala.
Ni tunu kwa nchi kuwa na Zitto
Kabwe. Ni kiongozi ambaye huwa hafichi hisia zake. Akiumizwa huwa hanyamazi.
HITIMISHO
Tunamhitaji Rais Magufuli kwa
nafasi yake na utashi wake wa kizalendo.
Tunamhitaji Lissu kwa jicho lake
la kuyasaka makosa ya Serikali na kuyaweka wazi.
Tunamhitaji Zitto kwa maono
mapana na hoja mbadala zenye tija kwa taifa.
Mwisho kabisa, Rais Magufuli,
Lissu na Zitto wote ni Watanzania na wanaipenda sana nchi yao. Hilo ndilo
ambalo naliona kwa wote hao.
Rais Magufuli anataka mabadiliko
makubwa kwenye nchi ili taifa linufaike kwa rasilimali zake, hii ni kwa sababu
Rais Magufuli anaipenda sana Tanzania yake.
Lissu anakosoa mbinu ambazo Rais
Magufuli anazitumia kwa sababu anaona zinaweza kuigharimu nchi. Lissu anajua
kuwa nchi haiwezi kubeba gharama bila yeye kuathirika. Hii ni kwa sababu Lissu
anaipenda sana Tanzania yake.
Zitto anatoa hoja za utatuzi wa
changamoto za sekta ya madini, akisahihisha hatua za Rais Magufuli kwa sababu
anaamini kwamba Rais Magufuli hapaswi kuachwa peke yake kwenye vita hii ya
uchumi kupitia madini ya Tanzania. Hii ni kwa sababu Zitto anaipenda sana
Tanzania yake.
Nawapenda sana hawa wazalendo wa
nchi hii.
Kila mmoja ana nia njema.
Ni vizuri kusikilizana na kukopeshana kama siyo kuazimana mawazo
ili kufikia mafanikio ya pamoja kama nchi.
Tanzania haina malaika, kwamba
akifanya jambo asikosolewe hata kama ni jema kiasi gani.
Wanaokosoa nao ni Watanzania wazalendo.
Vema kusikilizana.
Mwisho kabisa wote wanaipenda Tanzania.
Wasioipenda Tanzania wote wapo
kimya, hawana maoni, wala hawawezi kuingia kwenye malumbano, maana wanaogopa
'kuamsha dude', wakifunua vinywa watakumbushwa usaliti wao kwa nchi na wizi
waliofanya.
Kila mtu aachwe huru kutoa maoni
yake.
Nchi inawahitaji Rais Magufuli, Lissu na Zitto kwa wakati mmoja.
Ndimi Luqman MALOTO
No comments