WAZIRI LUKUVI ATISHIA KUMPASUA KITAMBI MKURUGENZI
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi,
William Lukuvi, amemtahadharisha Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Manispaa
ya Ilemela, John Wanga, kwamba endapo atashindwa kusimamia vema agizo la
urasimishaji makazi holela na uandaaji wa hati miliki kwa wananchi,
atatumbuliwa.
Alitoa tahadhari hiyo
juzi baada ya kusomewa taarifa ya utekelezaji wa urasimishaji na uandaaji wa hati za ardhi
ambako Halmashauri ya Ilemela imetekeleza kwa asilimia moja kwa kuandaa hati
834 huku viwanja vingine 16,000 vikiwa vimepimwa bila kuandaliwa hati.
Lukuvi
ambaye alionekana kukasirishwa na hali hiyo alisema kushindwa
kuandaliwa hati hizo ndani ya Halmashauri ya Ilemela ambayo ina
maofisa ardhi na watathmini zaidi ya 40
kmeisababishia hasara Serikali.
Alisema kazi hiyo
ingefanyika ilivyotarajiwa serikali ingepata
mapato ya Sh bilioni 2.5 kwa
mwaka lakini kilichopatikana ni Sh
bilioni 1.3 tu.
“Hakuna halmashauri
nchini iliyo na watumishi wengi wa idara
ya ardhi kama Ilemela na Nyamagana mara zote nimekuwa nikifikiria kuwahamishia
wilaya nyingine kama Geita kwa Mheshimiwa Rais, Dk. John Magufuli ambako hakuna hata mmoja.
“Lakini leo pamoja na wingi wenu mnaandaa hati 834
huku viwanja 16,000 mkishindwa kuvikamilisha kwa muda niliotoa.
“Sasa Mkurugenzi
nakuambia kwamba Serikali imewavumilia
vya kutosha na sasa kama hautabadilika kwa muda ambao nimekuongezea
kuanzia sasa hadi Juni 30, mwaka huu
tambua kwamba kitambi chako kitapata pancha.
“Wewe mwenyewe utajua
namna ya kuiziba pancha hiyo, hatuwezi kuimba wimbo huo huo kila mwaka.
“Kuna vitu vidogo vidogo vya hapa halmashauri mnavifinyia kazi lakini suala ambalo ni la
muhimu mnashindwa kukamilisha.
“Nilikuwa namuona
mkurugenzi ni mjanja lakini
anachokifanya hapa ni kama kutwanga maji kwenye kinu kwa sababu kodi ya ardhi
haikusanywi,” alisema.
Waziri alisema Halmashauri za Ilemela na
Nyamagana zinatakiwa zikamilishe hatua
hiyo Juni 30, mwaka huu atakapoifunga
rasmi na kutangaza ‘masterplan’ ya Jiji la Mwanza ifikapo Agosti.
Aliwataka wananchi
kutambua kuwa baada ya kufungwa
urasimishaji makazi haitatokea
tena fursa ya namna hiyo.
Alisema wananchi
ambao hawatakuwa na hati ya eneo analoishi watahesabika kama wavamizi, hivyo
watapoteza haki yao na maeneo hayo yatachukuliwa na Serikali kwa shughuli
nyingine.
Lukuvi alisema
Serikali kuu imetenga Sh bilioni 22 kwa ajili ya masterplan ya Mwanza ambayo itaanza kutekelezwa Agosti
mwaka huu, kazi ambayo itafanywa na wataalamu kutoka China.
No comments