WATUHUMIWA WA MAUAJI KIBITI WATIWA MBARONI
Mkuu wa Wilaya ya Rufiji, ambaye pia anakaimu
Wilaya ya Kibiti, Juma Njwayo, amesema
vyombo vya dola vimewakamata watu wengi wanaodaiwa kuhusika na uhalifu wa kuua
watu katika maeneo mbalimbali ya wilaya hizo.
Njwayo amesema licha ya
watuhumiwa hao kukamatwa, pia vyombo vya dola vinaendelea kuwasaka watuhumiwa
wengine wanaojihusisha na vitendo hivyo.
“Kuna watu wanaoshukiwa ambao
ni wengi wamekamatwa na wanaendelea kuhojiwa, kuna wengine wanatafutwa na
wakipatikana watahojiwa, lakini hawajakamatwa kwa maana ya kwamba imethibitika
wao ni wahalifu,” alisema.
Katika hatua nyingine,
aliwataka wananchi wa maeneo hayo waendelee kufanya shughuli zao, lakini kwa
tahadhari.
“Watu wanalima, wanaofanya
shughuli za Serikali wanafanya, lakini haya yanafanyika tunapata uthibitisho
kwa mfano wa hawa watu wanne waliouawa huku Rufiji, kwa hiyo hali iko hivyo.
Tunaomba watu sasa wafanye shughuli zao kwa tahadhari, wakiona mtu wasiyemjua
watoe taarifa katika vyombo.
“Pia kama wanazo taarifa
watuambie, sisi tunajua hawa watu wako kwenye jamii, haiwezekani mtu asiyekujua
wewe aje akupige risasi jioni, lazima awe anakujua na kama hakujui basi
anashirikiana na mtu anayekujua. Hivyo tunawasisitiza hawa wananchi wetu wawe
na tahadhari ya kiusalama,” alisema.
Alipoulizwa amebaini nini
katika matukio hayo yanayowalenga zaidi viongozi wa Serikali, alisema suala
hilo ni gumu na bado haijajulikana sababu ya uhalifu huo.
“Hatujui sababu ni nini, lakini
ni kweli watu wote waliopata hilo tatizo wapo askari, wapo viongozi ama ni wa
serikali ya vijiji au chama tawala,” alisema.
Awali, Njwayo alikiri wazi kuwa
wananchi katika maeneo hayo wanaishi kwa hofu kwa sababu matukio si ya kawaida.
“Lazima uhofu, yaani upo
nyumbani kwako unakula mtu anakuja anakupiga risasi, watu nao wanasikia mlio wa
risasi lazima wapate hofu, hilo ni jambo la kila mtu mwenye akili yake timamu
lazima ahofie.
“Lakini sisi kwa upande wetu wa
wilaya halitupendezi jambo hili, tuna hatua nyingi tunazichukua kwa
kushirikiana na Serikali Kuu kupambana na jambo hili,” alisema.
Kauli ya Njwayo imekuja siku
chache baada ya watu wasiofahamika kumuua Mwenyekiti mstaafu wa Chama Cha
Mapinduzi (CCM) Kijiji cha Muyui, Iddy Kirungi, huku mtoto wake, Nurdin
Kirungi, akipigwa risasi ya tumbo wilayani Kibiti.
Wauaji hao baada ya kutekeleza
unyama huo walitokomea kusikojulikana, hali inayotishia usalama wa raia na mali
zao, huku wengine wakilazimika kuzikimbia nyumba zao kwa hofu ya kupoteza
maisha.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani
limethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema linaendelea kuwasaka wahalifu
na kuimarisha ulinzi.
No comments