SAKATA LA VYETI FEKI : MATANGAZO YA KUPOTELEWA VYETI YAFURIKA KWENYE MAGAZETI
MATANGAZO
ya upotevu wa vyeti yameongezeka katika magazeti mbalimbali na kwa siku ya jana
pekee yalikuwapo 90.
Kitendo
cha matangazo hayo kuongezeka kimeibuka ikiwa imebaki siku moja kwa baadhi ya
watumishi wa Serikali wanaodaiwa kuwa na vyeti feki kutakiwa kukamilisha
mchakato wa kukata rufaa.
Taarifa
ya watumishi hao, ambao ni miongoni mwa 9,932 kutakiwa kukata rufaa ilitangazwa
wiki iliyopita na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya
Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dk. Laurean Ndumbaro, kutokana na kuamini
pengine wameonewa kutajwa katika orodha ya vyeti feki.
Baada
ya Dk. Ndumbaro kutoa taarifa hiyo, matangazo hayo yamekuwa yakiongezeka siku
hadi siku na yamekuwa yakihusisha zaidi upotevu wa vyeti vya kidato cha nne
vinavyodaiwa kuwa na utata kwa baadhi ya watumishi.
Miongoni
mwa waliotangaza matangazo hayo wamo wahadhiri wa vyuo vikuu na haijajulikana
kama nao wanahusika moja kwa moja katika uhakiki huo.
Pia
huenda matangazo hayo yakaongezeka zaidi baada ya kuwapo kwa taarifa ya
kutangazwa kwa orodha mpya ya watumishi wanaodaiwa kuwa na vyeti feki waliopo
katika taasisi na wizara zilizobaki, pindi mpango mwingine wa uhakiki wa vyeti
utakapokamilika.
Wakati
matangazo hayo yakiendelea kuongezeka kwa kasi magazetini, orodha ya rufaa hizo
inatarajiwa kutolewa kesho na Baraza la Taifa la Mitihani (NECTA).
Juzi
Dk. Ndumbaro alilithibitishia MTANZANIA Jumapili kuwa, awamu nyingine ya mpango
huo ipo katika hatua za mwisho na muda wote kuanzia sasa majina hayo
yatatangazwa.
Dk.
Ndumbaro alisema orodha hiyo mpya iliyopaswa kutangazwa Jumatano wiki hii
itatoka siku yoyote kuanzia kesho.
No comments