Wavuvi 53 Zanzibar waliozama waokolewa

Watu 53 wanaosadikiwa kuwa wavuvi
wamenusurika kifo baada ya boti yao kukumbwa na dhoruba na kuzama baharini eneo
la Mkokotoni, Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Akizungumzia tukio hilo, Kamanda wa
Polisi wa mkoa huo, Hasina Ramadhan Tawfiq alisema boti hiyo inafahamika kwa
jina la Advantage na watu hao waliokolewa, na baada ya matibabu katika
hospitali za Tumbatu na Kivunge waliruhusiwa kurejea makwao.
Hasina alisema taarifa za tukio hilo
walizipata juzi jioni baada ya kuokolewa kwa mmoja wao na meli ya Azam Link
iliyokuwa ikitokea Pemba kwenda Unguja na kuwa boti hiyo ilizama saa nne
asubuhi. Kamanda huyo alisema jitihada za uokoaji zilifanywa na vikosi vya
KMKM, ZMA na Polisi.
Mvuvi aliyeokolewa, Khatib Khamis
ambaye ni mkazi wa Mtoni alisema chanzo cha tukio hilo ni upepo mkali
ulioambatana na mawimbi yaliyosababisha chombo chao kupinduka. Alisema kabla ya
tukio hilo walikuwa wanatokea Mtoni kuelekea Kisiwa cha Tumbatu kuvua.
No comments