Video: kauli ya Prof. Kitila Mkumbo baada ya kuapishwa na Rais Magufuli

Rais Dkt. John
Pombe Magufuli, leo tarehe 05 Aprili, 2017 amewaapisha viongozi aliowateua
kushika nyadhifa mbalimbali.
Hafla ya kuapishwa
viongozi hao imefanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na Makamu wa
Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan.
Moja ya viongozi
walioapishwa ni Prof. Kitila Alexander Mkumbo kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya
Maji na Umwagiliaji.
Prof. Mkumbo
aliyekuwa mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na mmoja wa wanachama wa
chama cha ACT Wazalendo, baada ya kuapishwa aliongea maneno machache
akimshukuru Rais Magufuli kwa kuuona umuhimu wake na kumteua kuwa katibu katika
wizara hiyo.
Aidha
amemuhakikishia Rais kuwa ataifanya kazi yake kwa weledi mkubwa na taifa
litarajie matokeo makubwa katika utendaji wake.
“Kazi yetu na
jukumu letu kubwa ni kuhakikisha kuwa sera ya umwagiliaji tunaitekeleza”
alisema.
Vilevile aliongeza
kuwa katika maisha yake yote akiwa mhadhiri, amekuwa ni mtu wa kuhoji maswali
mbalimbali kwa serikali ili kuhakikisha kuwa wanafanya kazi yao kwa weledi.
“Maisha yangu yote
mpaka hapa nilipo nimetumia muda wangu mwingi kuhoji na kuuliza maswali hasa
kwa serikali. Nimepata fursa sasa ya kushiriki kikamilifu, badala ya kuhoji
nina kazi ya kujibu maswali ya serikali. Mh rais nakuahidi kuwa nitajibu hoja
mbalimbali za serikali” alisema.
Viongozi wengine
walioapishwa leo ni pamoja na Dkt. Ave Maria Emilius Semakafu kuwa Naibu Katibu
Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Baraka Haran Luvanda kuwa
Balozi wa Tanzania nchini India, Mhe. Sylvester Mwakinyuke Ambokile kuwa Balozi
wa Tanzania nchini Afrika Kusini na Bw. Charles Edward Kichere kuwa Kamishna
Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Hapa chini ni video
ya Prof. Kitila Mkumbo akiongea Ikulu jijini Dar es salaam leo mara baada ya kuapishwa
na Mh. Rais Magufuli.
No comments