Kutoka Dodoma: Madiwani Wamng'oa Meya Kwa Kutokuwa Na Imani Naye
MADIWANI wa Manispaa ya Dodoma wamemwondoa
Meya wao, Jafari Mwanyemba kwa kumpigia kura ya kutokuwa na imani naye kutokana
na kumtuhumu kuhusika na tuhuma mbalimbali zikiwamo za ubadhirifu wa fedha.
Kura hizo zilipigwa mjini hapa kwenye Mkutano
Maalumu wa Madiwani wa kujadili tuhuma dhidi ya Meya Mwanyemba.
Kati ya madiwani wa manispaa hiyo 56, 47 ndio
walipiga kura ya kutokuwa na imani naye dhidi ya kura nne zilizodai kuwa na
imani naye, wakati kura moja iliharibika na madiwani wanane hawakupiga kura.
Akitangaza matokeo hayo, Mkurugenzi Mtendaji
wa Manispaa, Godwin Kunambi alisema kuanzia saa 8.30 adhuhuri hiyo, Mwanyemba
si Meya wa Manispaa ya Dodoma na kutokana na kanuni za manispaa, Naibu Meya
Jumanne Ngede ndiye atakayekuwa akiongoza hadi uchaguzi wa kuziba nafasi
utakapofanyika miezi miwili kuanzia sasa.
Alisema kutokana na kanuni za halmashauri hiyo
namba 4 (8), baada ya Tume iliyoundwa na Mkuu wa Mkoa kurudisha ripoti kwa
mkurugenzi katika kipindi cha siku 14, alitakiwa kuwasilisha kwenye mkutano
maalumu wa madiwani kwa uamuzi wa tuhuma dhidi ya meya huyo ambapo madiwani
wameamua kumng’oa kwa kupigia kura.
Kutokana na kupigwa kura ya kumng’oa, kanuni
za halmashauri zinamruhusu aliyekuwa Meya wa Manispaa ndani ya mwezi mmoja
kukata rufaa kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za
Mitaa.
No comments