Nimesoma na kuona katika vyombo mbalimbali vya habari kuhusu vurugu
zilizotokea tarehe 22 Aprili, 2017 katika hoteli ya Vina, Mabibo hapa Dar es
salaam, zinazosemekana kuhusisha wanachama wa CUF.
Ni ukweli usiopingika kuwa, suala la mgogoro wa uongozi
katika chama cha CUF lipo mahakamani, lakini nikiwa msimamizi wa Sheria ya
Vyama vya Siasa na kutambuliwa na jamii kuwa ni mlezi wa vyama vya siasa;
nimelazimika kuwasihi wadau wa siasa hususani wanachama wa chama cha CUF,
kutambua kwamba, kuwapo kwa shauri mahakamani siyo fursa ya kufanya vitendo vya
uvunjifu wa amani, kwani jambo hili ni uvunjifu wa sheria na linaleta sura mbaya
kwa jamii.
Hivyo, ninalaani vurugu hizo, ambazo zilionekana kuvunja
amani na utulivu na watu kuumizwa, tofauti na tunu zetu za taifa za amani na
utulivu. Pia, nawaasa wanachama wa CUF pamoja na tofauti walizonazo, madhali
masuala haya yapo mahakamani hebu tuheshimu utawala wa Sheria.
Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa na hata Jeshi la Polisi
lipo kushughulikia malalamiko yoyote yanayohusu uendeshaji na shughuli za chama
chochote cha siasa. Hivyo, hakuna haja ya wanachama wa chama cha CUF kukiuka
taratibu za kuendesha chama hicho au kujichukulia Sheria mkononi.
Aidha, ninaviasa vyama vya siasa kuelewa kuwa havipo juu ya
Sheria, vinapaswa kuheshimu na kufuata Sheria za nchi, ikiwamo kutunza amani na
utulivu tulionao.
Mwisho, ninaomba vyombo vya ulinzi na usalama katika nchi
yetu kulifanyia kazi tukio hilo, ili wahusika wafahamike na kuchukuliwa hatua
za kisheria. Kwa upande wa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa inayosimamia
utekelezaji wa Sheria ya Vyama vya Siasa, haitasita kuchukua hatua stahiki kwa
mujibu wa Sheria.
Jaji Francis S.K.
Mutungi
MSAJILI WA VYAMA VYA SIASA
24 Aprili, 2017
No comments