BUNGE LAKATAA MAJINA YA WAGOMBEA WA CHADEMA NA CUF KWENDA KUGOMBEA NAFASI YA UBUNGE WA AFRIKA MASHARIKI (EALA)
Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limekataa majina ya
wagombea wa CHADEMA na CUF kwenda kugombea nafasi ya Ubunge wa Afrika Mashariki
(EALA) baada ya kukutwa na mapungufu katika fomu zao.
Hatua hiyo imekuja baada ya wagombea hao kuonekana na mapungufu
mbalimbali yaliyobainika kwenye nyaraka zao a uteuzi yakiwa yamekiuka masharti
ya Ibara ya 50 ya Mkataba wa Kuanzishwa kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Ibara
ya 67 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Kifungu cha 4(4) cha
Sheria ya Uchaguzi wa wajumbe wa Bunge la Afrika Mashariki ya Mwaka 2011
iliyotungwa na Bunge la Afrika Mashariki.
Aidha taarifa hiyo imesema CHADEMA uteuzi wao haukuzingatia
jinsia, lakini pia hawajaambatanisha fomu za maombi ya wagombea, orodha ya
waombaji pamoja na fomu ya matokeo ya kura.
Huku CUF wakiwa wametuma fomu za uteuzi wa wagombea zikiwa
zimewasilishwa na mamlaka mbili tofauti, wagombea wawili hawana uthibitisho wa
uraia wao, fomu za uthibitisho wa hiari ya kugombea haikuwepo kwa wagombea
wote, orodha ya waombaji haipo kwa mgombea mmoja, fomu ya matokeo ya kura kwa
wagombea haikuwepo pamoja na fomu ya mahudhurio kwa mgombea mmoja kutotimia.
Kutokana na mapungufu hayo msimamizi wa Uchaguzi Dr. Thomas D.
Kashililah amesema ameshindwa kufanya uteuzi huo huku akiwataka kurekebisha
mapungufu yaliyobainishwa kabla ya saa 7 mchana, Aprili 4 ofisini kwake mjini
Dodoma.
Kwa upande mwingine amewashukuru wadau wote hususani vyama vyote
vya siasa nchini kwa ushirikiano mzuri waliyompa katika zoezi zima la mchakato
wa uteuzi wagombea pamoja na vyombo vya habari kwa ujumla.
No comments