RAIS MAGUFULI: MARUFUKU MCHANGA KUSAFIRISHA NJE YA NCHI
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, amepiga marufuku
usafirishaji wa mchanga wa madini nje ya nchi na ametaka mchanga wote ufanyiwe
uyeyushaji hapa hapa nchini.
Rais
Magufuli ametoa katazo hilo leo wakati akiweka jiwe la msingi la kiwanda cha
kutengeneza vigae (Tiles) cha Kampuni ya Goodwill Tanzania Ceramic Limited
kilichopo katika Wilaya ya Mkuranga Mkoani Pwani.
Akizungumza
baada ya kutembelea kiwanda hicho, Mhe. Rais Magufuli ameishukuru Menejimenti
ya kiwanda hicho kwa uwekezaji huo na ameelezea kufurahishwa kwake na kutumika
kwa teknolojia ya kuyeyusha mchanga wa kutengenezea vigae.
"Nchi
hii tumechezewa vya kutosha, sasa nyinyi hapa mnayeyusha mchanga kwa kuuchemsha
hadi nyuzi joto 1,000 wakati wengine wanasafirisha mchanga nje ya nchi wakati
uchemshaji wake hauhitaji kufika hata nyuzi joto 1,000, naiagiza Wizara ya
Viwanda, Biashara na Uwekezaji na Wizara ya Nishati na Madini kuwa kuanzia sasa
ni marufuku kusafirisha mchanga nje ya nchi" amesisitiza Mhe. Rais
Magufuli.
Kiwanda
hicho kikubwa Afrika Mashariki na Kati ambacho ujenzi wake umegharimu Dola za
Marekani Milioni 50 kwa awamu ya kwanza kitakuwa na uwezo wa kuzalisha mita za
mraba 80,000 za vigae kwa siku, kitazalisha ajira za moja kwa moja 1,000 na
ajira zisizo za moja kwa moja 2,000.
Akizungumza
kabla ya kuweka jiwe la msingi la kiwanda hicho Katibu Mkuu wa Wizara ya
Viwanda, Biashara na uwekezaji Dkt. Adelhelm Meru amesema pamoja na kiwanda
hicho, tangu Serikali ya Awamu ya Tano iingie madarakani jumla ya viwanda 2,169
vinavyojumuisha viwanda vidogo, vya kati na vikubwa vimesajiliwa na Kituo cha
Uwekezaji Tanzania (TIC) na vipo katika hatua mbalimbali za kukamilika.
Naye
Balozi wa China hapa nchini Mhe. Dkt. Lu Youqing amempongeza Mhe. Rais Magufuli
kwa kutilia mkazo juhudi za kukuza uchumi zilizowezesha Tanzania kuwa miongoni
mwa nchi zenye uchumi unaokuwa kwa kasi kubwa Barani Afrika na amebainisha kuwa
China itaendelea kushirikiana na Tanzania kuendeleza uwekezaji nchini Tanzania
ikiwemo kujenga viwanda.
"Mhe.
Rais kwa mujibu wa takwimu za TIC mpaka mwisho wa Juni 2016 uwekezaji wa moja
kwa moja kutoka China umefikia Dola za Marekani Bilioni 6.6 na umezalisha ajira
za moja kwa moja kwa Watanzania 150,000 na zisizo za moja kwa moja 450,000 na
kiwanda hiki cha Goodwill Tanzania Ceramic Limited kimejengwa na wawekezaji
kutoka China, vipo viwanda vingine vingi vinajengwa, Mbunge wa Mkuranga
ameniambia kuwa kuna viwanda zaidi ya 50 vya Wachina vinavyojengwa hapa
Mkuranga, nimefurahi sana kuona karibu kila sekta Watanzania wanafurahia
ushirikiano wa Tanzania na China" Amesema Balozi Dkt. Lu Youqing.
No comments