WAZIRI MKUU AKABIDHIWA KAZI YA KUPAMBANA NA DAWA ZA KULEVYA
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli amemkabidhi Waziri
Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa kazi ya kuzuia na kupambana na dawa za kulevya akiwa
kama Mwenyekiti wa Tume ya Kudhibiti Dawa hizo nchini.
Rais
Magufuli ameyasema hayo leo Ikulu Jijini Dar es Salaam wakati akiwaapisha
Kamishna Jenerali wa Jeshi la Uhamiaji, Anna Peter Makakala, Kamishna Mkuu wa
Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya, Rogers William Sianga pamoja
na mabalozi watatu Mhe. Omary Yusuph Mzee, Mhe.Joseph Edward Sokoine pamoja na
Mhe. Grace Aron Mgovano aliowateua hivi karibuni.
Dkt.
Magufuli amesema kuwa Waziri Mkuu anatajwa kwenye Sheria Na.5 ya mwaka 2015
kuwa ni Mwenyekiti wa Tume hiyo ambapo Wajumbe wake ni Waziri wa Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano, Waziri wa Mambo ya Ndani, Waziri wa Elimu ana Mafunzo
ya Ufundi, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Waziri wa Fedha na Mipango, Waziri wa Afya,
Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto pamoja na Waziri wa Kilimo, Mifugo
na Uvuvi.
“Nalipongeza
sana Bunge la kipindi cha mwaka 2010 – 2015 chini ya Spika mstaafu, Mhe. Anne
Makinda lililopitisha Sheria hii baada ya kuona sheria za mwanzo za kupambana
na dawa za kulevya hazina nguvu hivyo Wabunge wa wakati ule walisimama kwa
pamoja bila kujali itikadi za vyama vyao wakapitisha sheria hii,” alisema Dkt.
Magufuli.
Aidha,
Dkt. Magufuli amempongeza Rais Mstaafu Dkt. Jakaya Kikwete kwa kusaini sheria
hiyo haraka mara baada ya Bunge hilo kuipitisha kwa sababu alijua madhara ya
dawa za kulevya katika nchi yetu.
Amefafanua
kuwa sheria imeeleza wazi katika kifungu cha 10 cha Sheria Na.5 ya mwaka 2015
kuwa jukumu la kupambana na dawa za kulevya linasimamiwa na Serikali pekee yaani
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar, Makamo wa Rais, Waziri Mkuu, Mawaziri, Wakuu wa Mikoa na Wilaya
pamoja na Wakurugenzi wa Halmashauri za Wilaya au mtu yoyote atakayekuwa
amepewa mamlaka ya kusimamia Serikali.
Kwa
upande wake Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa amesema kuwa Taifa limeendelea
kushuhudia kizazi chetu kikiendelea kudidimia kwa sababu ya matumizi ya dawa za
kulevya na Serikali kwa mipango yake imeendelea kukemea, kudhibiti na kuchukua
hatua mbalimbali dhidi ya wazalishaji, wasambazaji, wauzaji na watumiaji wa
dawa hizo.
“Jambo
hili limeleta athari kubwa sana kwani vijana wetu wengi wamepoteza uwezo wa
kujisimamia katika shughuli zao za maendeleo kwa sababu baada ya matumizi
tumeona athari kadhaa zikiwezo za kudhoofishwa kwa mwili, uwezo wa kutafakari
pamoja na kutoweka kwa uwezo wa kufanya kazi,”alisema Waziri Mkuu Majaliwa.
Waziri
Mkuu Majaliwa ameongeza kuwa Taifa hili la Watanzania kwa kiasi kikubwa
linawategemea vijana waweze kuleta msukumo wa maendeleo ndani ya nchi hivyo
jambo hili likiachiwa linaweza kuleta athari kubwa katika ukuaji wa uchumi na
maendeleo yetu kwa ujumla wake.
Alisisitiza
kuwa vita hii ilianza, inaendelea na itaendelea kupiganwa hadi imalizike hivyo
Watanzania hawana budi kuunga mkono jitihada zozote zinazofanywa na Serikali
kuhakikisha wanatokomeza uzalishaji, usambazaji, uuzaji na matumizi yake kwa
namna yoyote ile, kila mmoja anatakiwa kushiriki kikamilifu ili kubaini
matumizi ya dawa za kulevya ndani ya nchi hii.
No comments