Breaking News

WAKAZI WA MIJINI WANAOMILIKI MAENEO YASIYO NA HATI KUTOZWA KODI


Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO.

Serikali imejipanga kuwatoza kodi wakazi wanaomiliki maeneo yaliyopo mijini ambayo hayana hati wala ofa kwa viwango vile vile ambavyo wakazi wenye hati wanatozwa.

Tamko hilo limetolewa leo Jijini Dar es Salaam na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari juu ya ulipaji wa kodi za ardhi.

Waziri Lukuvi amesema kuwa wizara hiyo inaendelea na ukaguzi wa ardhi ambapo mwanzoni ilianza na ukaguzi wa mashamba yanayomilikiwa bila kuendelezwa lakini kwa sasa imegundulika kuwa kuna maeneo makubwa mijini yasiyokuwa na hati yanamilikiwa na wananchi na kusababisha eneo kubwa la ardhi kutumika bila kulipiwa kodi.

“Kwa muda wote huo Serikali imekuwa haiwatozi kodi wananchi wanaomiliki maeneo mijini bila kuwa na hati hivyo, kuanzia sasa Serikali kupitia wizara yangu itawatoza kodi watu wote nchini wanaomiliki maeneo ndani ya miji hata kama hawana hati au ofa ili mradi wana karatasi za mauziano ya ardhi,”alisema Lukuvi.

Ameongeza kuwa watu wote waliopo mjini ambao wana ardhi lakini hawana hati wala ofa wapeleke taarifa zao za maeneo wanayoyamiliki  kwa maafisa wateule wa ardhi kwenye halmashauri zao ili yaweze kujulikana ili kuanza kulipiwa kodi.

Amefafanua kuwa kila mwananchi lazima aende na kielelezo kinachoonyesha umiliki wake katika eneo husika na akatamke mwenyewe ukubwa wa eneo alilonalo ili kama itatokea  amedanganya ukubwa wa eneo lake na wizara ikagundua basi eneo hilo lililozidi litamilikiwa na Serikali bila kulipa fidia yoyote.

Aidha, Waziri Lukuvi amesema kuwa kuanzia mwezi Julai mwaka huu wizara itaanza kuwatoza kodi wananchi wote waliojenga mjini katika maeneo ambayo viwanja vyake havijapangwa wala kupimwa kwani watu hao wanaishi mjini na wanatumia miundombinu ya umma inayojengwa kwa kutumia kodi za wananchi.

“Ardhi ya Tanzania inayotumika ni zaidi ya asilimia 70 lakini eneo linalolipiwa kodi halizidi asilimia 11 na wengi wao wanaitumia isivyo rasmi na hawalipi kodi kwa Serikali hivyo kila mtu mwenye ardhi awe na nyaraka rasmi au isiyo rasmi wote wanatakiwa kulipa kodi ya ardhi na baada ya miezi 6 kutoka sasa, eneo ambalo halitakuwa limesajiliwa litachukuliwa na kumilikiwa na Serikali,”alimalizia Lukuvi.

Ni lazima kuwatambua watu wote wanaomiliki ardhi kisheria, kimila au kwa namna nyingine yoyote ili kufahamu ardhi inamilikiwa na nani na inatumika kwa matumizi gani.

No comments