MAHAKAMA YAICHARUKIA SERIKALI KESI YA GODBLESS LEMA. YAHOJI SABABU ZA MBUGE HUYO KUNYIMWA DHAMANA.
Mwenyekiti wa kikao cha jopo la Majaji watatu wa Mahakama ya Rufaa, kinachoendelea Arusha, Bernard Luanda, leo amegeuka mbogo kwa wanasheria wa serikali kwa kitendo cha kumnyima Mbunge wa Arusha Mjini Godbless Lema dhamana kwa lengo la kumnyima haki.
Akizungumza
Mahakamani hapo leo mbele ya majaji wenzake Stella Mugasha na Jaji Kipenka
Mussa, Luanda amesema haipendezi na haingii akilini mtu (Lema) kushikiliwa kwa
miezi minne bila sababu kwa misingi ya kumnyima haki.
“Tunaomba
ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa serikai (DPP) muwe makini sana maana mnatufanya
wanasheria wote hatuna akili na mnachafua Mahakama, kwa hali ya kawaida mtu
mumshikilie kwa misingi ya kisheria, lakini katika kesi hii tumepitia jalada
hatujaona kitu chochote cha kumshikilia Lema hadi leo na imetushitua sana,”
alisema huku akishauriana na wenzake mara kwa mara kwa masikitiko.
Aliendelea
kusema kuwa ofisi ya DPP inaitia najisi taaluma hiyo, kitu kipo wazi ila
wanafanya vitu vya ajabu na havipendezi.
Alihoji
jaji Luanda kuwa “Tumesoma faili lote tunashangaa hivi kweli ofisi ya
mwanasheria mkuu ina wanasheria kweli na kama wapo kwa nini huyu mtu (Lema) awe
ndani mpaka leo?”.
Alisema
kwa kuwa mikono yao kisheria imefungwa hawawezi kufanya chochote kwa leo na
kuwataka Mawakili upande wa Lema kurudi Mahakama Kuu, kuendelea na maamuzi ya
dhamana.
Hali
hiyo ilitokana na Wakili wa serikali Faraja Nchimbi kusimama mahakamani hapo na
kuomba kuiondoa rufaa hiyo kwa madai kuwa ipo nje ya uwezo wake.
“Waheshimiwa
Majaji baada ya timu yetu ya wanasheria kupitia kwa kina rufaa hii kwa sababu
zisizozuilika tumeona hatupo tayari kuendelea na rufaa hii, maana hatukupeleka
kusudio (Notisi) kwa msajili muda ulipita, hivyo tunaomba kuiondoa na uamuzi wa
kuiondoa rufaa hii tumeufikia Ijumaa muda uliisha kuja mahakamani,”. Alisema
Nchimbi.
Baada
ya kuwasilisha ombi hilo, Wakili wa Lema Peter Kibatala, alisimama na kusema
upande wao hawana pingamizi ila waliomba hoja za awali za rufaa hiyo ziondolewe
Mahakamani hapo bila kunakiliwa.
Baada
ya ombi hilo Jaji Kipenka Mussa alipokea kwa niaba ya Majaji wenzake na
kukubali ombi la kuiondoa rufaa hiyo namba 9/2017.
Aidha
Jaji Luanda alimkaribisha jaji Stella Mugasha pia kuongea kwa niaba yao ambapo
alisema mahakama imekubali ombi la pili la kuiondoa rufaa namba 10/2017, baada
ya Wakili Paul Kadushi kuomba kuiondoa pia.
Wakili
wa Lema Peter Kibatala, alilazimika kusimama tena Mahakamani hapo kusema kuwa
upande wao unasikitika kuona ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na DPP wanatumia
Mahakama kwa njia ya kumnyima haki mteja wao, hivyo aliomba mahakama hiyo
iwatatulie tatizo la kisheria lililojitokeza hadi mteja wao awe ndani hadi
sasa.
Kibatala
aliongea hayo huku akishindwa kujizuia na kumwaga chozi la huzuni mahakamani
hapo mbele ya Majaji hao.
No comments