KAULI YA HASHIM RUNGWE MARA BAADA YA KUTOKA KUMJULIA HALI GODBLESS LEMA GEREZANI
Mwenyekiti wa Chama cha Ukombozi wa Umma (Chauma),
Hashim Rungwe, amemtembelea Mbunge wa Arusha Mjini, Godbles Lema (Chadema),
ambaye bado yuko mahabusu katika Gereza
la Kisongo mkoani Arusha.
Akizungumza
na waandishi wa habari mjini Arusha jana
baada ya kuonana na mbunge huyo, Rungwe alisema baadhi ya matatizo yanayotokea
kwenye jamii yanasababishwa na baadhi ya watawala.
Alisema
hali hiyo imekuwa ikiibua chuki miongoni mwa wananchi jambo ambalo si zuri na linahitaji kukemewa.
Kiongozi
huyo alimtembelea Lema akiwa amefuatana
na viongozi mbalimbali akiwamo Makamu Mwenyekiti wa Chauma, Kayumbo
Kabutali na wabunge wa Bukoba Mjini,
Wilfred Lwakatare na Moshi Vijijini, Antony Komu, wote wa Chadema
“Historia
ya zamani inatufunza matatizo yanayotokea katika jamii yanachangiwa na mambo
yanayotendwa na baadhi ya watawala
ambayo yanaleta chuki.
“Na
chuki siyo kitu kizuri kwa sababu inazidi kuwa kubwa kwenye mioyo ya watu hata
kama wako kimya,”alisema na kuongeza:
“Hili
limewahi kutokea enzi za mitume hata Nelson Mandela aliwekwa ndani na alipotoka
dunia nzima iliamka hivyo tunaona kuna baadhi ya watu wanawekwa ndani bila
sababu ya msingi, natoa wito kwa wenye mamlaka kuangalia suala hili.”
Mwenyekiti
huyo alisema ni wakati wa watanzania wote kwa ujumla kupigia kelele suala hilo
kwa vile Mbunge ambaye ni mwakilishi wa
wananchi, anazuiliwa kwa makosa yenye dhamana jambo la kukemewa.
“Tumekuja
Arusha kumuangalia Lema kwa sababu ni
mwenzetu na tuna masikitiko na kama walifikiri wakimuweka Lema ndani
wanamsimamisha au kumkomesha, wanamkomaza kisiasa.
“Anapata
ujasiri wa aina Fulani kwa sababu
haelewi kwa nini yuko ndani, wangemkuta na malori matatu ya silaha
sawa,” alisema.
Mbunge
wa Bukoba Mjini alisema ameridhishwa na kupata matumaini na hali ya mbunge huyo
kwa vile ni yuleyule na ameongeza
ujasiri wa kulisema lile analoamini.
Naye
Mbunge wa Moshi Vijiji, Antony Komu,
alisema Lema ameomba wabunge wote bila kuangalia itikadi za vyama vyao
wanapaswa kuwa makini wakati wa utungaji wa sheria.
Alisema kutokana na baadhi ya upungufu wa sheria
kuna watu wako gerezani kwa muda mrefu.
Alisema katika gereza hilo asilimia kubwa wako
gerezani kwa muda mrefu kutokana na upungufu wa sheria mbalimbali.
No comments