KITWANGA ATISHIA KUONGOZA WANANCHI KUNG'OA MITAMBO YA MAJI ZIWA VICTORIA
Mbunge wa Misungwi
(CCM), Charles Kitwanga, amesema yuko tayari kuwahamasisha wananchi wa jimbo
lake kwenda kuing’oa ama kuizima mitambo ya kusukuma maji Ziwa Victoria
kupeleka mkoani Shinyanga ikiwa maji hayatafika jimboni kwake.
Kitwanga alitoa kauli hiyo bungeni jana alipokuwa akiuliza
swali la nyongeza.
Mbunge huyo alisema wananchi wa jimbo lake katika Vijiji vya
Ihelela Kashwasa, walishapewa ahadi tangu mwaka 2008 kuwa wangeunganishiwa maji
kutoka katika mtambo wa kusukuma maji kutoka Ziwa Victoria kwenda Shinyanga,
lakini hadi sasa ahadi hiyo haijatekelezwa.
“Ahadi hii ilitolewa na aliyekuwa Rais wa wakati huo, Jakaya
Kikwete, lakini kila siku ni ahadi bila utekelezaji. Kweli nitawasindikiza
wananchi wangu kuzima mitambo ili maji yasipelekwe Shinyanga, nasema kweli
nitafanya hivyo,” alisisitiza Kitwanga.
Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji,
Isaack Kamwelwe, alikiri kuwa Rais wa awamu ya nne alitoa ahadi hiyo mwaka 2008
kwamba wananchi wa maeneo ya Ihelela wataunganishiwa maji kutoka bomba la Ziwa
Victoria.
Hata hivyo, Kamwelwe alimuomba mbunge huyo asihamasishe watu
kuzima mitambo hiyo wakati wowote badala yake wavute subira.
Katika swali la msingi la Mbunge wa Kasulu Mjini, Daniel
Nsanzugwako (CCM), alitaka kujua Mto Malagarasi una ujazo gani wa maji na kama
yanatosheleza mahitaji.
Akijibu swali hilo, Naibu Waziri Kamwelwe alisema serikali
imepanga kutekeleza miradi mbalimbali kwa kutumia Mto Malagarasi ikiwamo mradi
wa maji kwa ajili ya miji ya Urambo, Kaliua pamoja na kilimo cha mwagiliaji na
uzalishaji umeme wa megawati 44.5.
“Wakati wa masika, mto huo unakuwa na maji yanayotiririka
kwa mita za ujazo 55 kwa sekunde na wakati wa kiangazi unakuwa na mita za ujazo
40 kwa sekunde," alisema.
No comments