KUTOKA BUNGENI: MBOWE NA NAIBU SPIKA DR TULIA NDANI YA BIFU JIPYA
Mvutano umeibuka bungeni kati ya Kiongozi wa Kambi
Rasmi ya Upinzani, Freeman Mbowe na Naibu Spika, Dk Tulia Ackson baada ya
Mbunge huyo wa Hai kumwuliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa swali lililopingwa na
Naibu Spika kwa maelezo kuwa ni la kisheria si la kisera.
Sakata
hilo liliibuka asubuhi katika kipindi cha maswali kwa Waziri Mkuu, baada ya
Mbowe kuhoji sababu za Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema kusota rumande kwa
kukosa dhamana, Peter Lijualikali wa Kilombero anayetumikia kifungo cha miezi
sita gerezani na wanachama wengine wa Chadema wanaokabiliwa na mashitaka
mbalimbali.
Mbowe
alimtaka kiongozi huyo wa shughuli za Serikali bungeni, aeleze kama ni sera ya
Serikali kuua vyama vya upinzani, huku akisema Rais John Magufuli alipata
kutamka kuwa atavimaliza vyama vya upinzani kabla ya mwaka 2020.
Kwa
maswali hayo, Dk Tulia alimtaka Waziri Mkuu kujibu swali linalohusu sera na
kuachana na yanayogusa masuala ya kisheria.
Jambo
hilo liliwafanya wabunge wa Upinzani huku wakipiga meza kwa takribani dakika
tano kupinga, wakimtaka Naibu Spika aache Waziri Mkuu ajibu swali hilo.
Katika
swali lake la msingi, Mbowe alisema wakati jana ikiwa ni Siku ya Haki Duniani,
imepita miezi mitatu tangu Lema aanze kusota rumande huku akinyimwa dhamana
licha ya kuwa iko wazi.
Pia
alisema Lijualikali anatumikia kifungo cha miezi sita jela kwa kosa la kisiasa
sambamba na mwenyekiti wa chama hicho wa mkoa wa Lindi, Suleiman Mathew
aliyefungwa miezi minane na madiwani zaidi ya sita na viongozi wengine 215 nao
wakifungwa au kuendelea na mashitaka huku zikifanyika hila za kuidhoofisha CUF.
“Haya
yanayoendelea katika Serikali ambayo ni kinyume na utamaduni na mazoea yetu
kama Taifa, je ni utekelezaji wa sera ya kuua upinzani chini ya Rais Magufuli?”
Alihoji Mbowe.
Kabla
ya Waziri Mkuu kujibu swali hilo, Dk Tulia aliingilia kati na hali kuwa hivi:
Dk
Tulia: Katika swali lako kuna masuala ya kisera na kisheria. Maswali
yanayomhusu Lema na Lijualikali na madiwani sita ni ya kisheria, hayo kuhusu
leo (jana) kuwa siku ya haki duniani, Waziri Mkuu anaweza kuyajibu.
Majaliwa:
Nakanusha, Rais hajawahi kutangaza kuvifuta vyama vya upinzani, nchi inaongozwa
kwa sheria, kanuni na taratibu na kuna Bunge, Serikali na Mahakama. Hakuna
mhimili unaoingilia mhimili mwingine. Jambo lililopo mahakamani halizungumzwi
kokote, siwezi kuzungumzia hilo.
Mbowe:
Kwa kuwa Rais anaonekana kuvunja Katiba ikiwa ni pamoja na kupiga marufuku
mikutano ya vyama vya siasa, je tukileta ushahidi kuwa Rais amekusudia
kuumaliza upinzani kabla ya 2020, Waziri Mkuu utakuwa tayari kuwajibika kwa
kujiuzulu?
Dk
Tulia: Mbowe swali lako la maelezo ya jumla, yako sawasawa ila la kumtaka
Waziri Mkuu kuwajibika si la kisera, kuwajibika si sera uliza swali la kisera.
Mbowe:
Labda swali langu nilielekeze kwa Naibu Spika (Dk Tulia). Swali langu lilikuwa
la mwendelezo ambalo hutokana na majibu ya msingi yaliyotokea. Kama kulikuwa na
msingi wa kisera kwenye swali la msingi, swali la mwendelezo linakwenda
kutokana na majibu yaliyotolewa. Waziri Mkuu aseme tu kama yupo tayari
kujiuzulu tukileta ushahidi.
Katika
maelezo yake, Dk Tulia alitaka Mbowe ajikite katika swali la kisera jambo
ambalo Mwenyekiti huyo wa Chadema alipinga na kusisitiza kuwa huenda mambo
yanayofanyiwa wapinzani, wabunge, mawaziri Serikali inayafurahia.
No comments