ASKOFU MOKIWA AKUBALI YAISHE, AIFUTA KESI YAKE MAHAKAMANI
Aliyekuwa Askofu wa Kanisa la Anglikana Jimbo la Dar es
Salaam, Valentino Mokiwa, amewasilisha barua mahakamani akiomba kuondoa kesi
aliyoifungua akipinga kustaafishwa kwa nguvu ili wakamalizane katika nyumba ya
maaskofu.
Mokiwa
anataka kuondoa kesi hiyo ya madai namba 20 ya mwaka huu aliyofungua dhidi ya
Askofu Mkuu wa Makanisa ya Anglikana Tanzania, Mhashamu Dk. Jacobe Chimeledya
na Bodi ya Wadhamini ya kanisa hilo.
Askofu
Mokiwa alifungua kesi hiyo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na iko mbele
ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba.
Akiieleza
mahakama, Wakili wa wadaiwa, Gabrieli Masinga alidai alipokea barua kutoka kwa Wakili wa Askofu
Mokiwa, Wakili M.B. Kabunga ikiwaelekeza kuwa kesi iliitwa jana kwa sababu
waliwasilisha barua ya kuomba kuiondoa mahakamani.
Alidai
barua hiyo ilieleza sababu za kuondoa kesi hiyo ni kutokana na juhudi za
kutatua mgogoro huo katika nyumba ya maaskofu.
“Wanaomba
kuondoa kesi wapate muda wa kujadiliana
kwa sababu juhudi haziwezi kufanyika
bila kesi hiyo kuondolewa mahakamani,”alidai.
Hakimu
Simba alisema barua hiyo hajaiona na kesi hiyo ilipangwa Februari 28 hivyo
kuwapo kwao jana mahakama hakutambui.
“Leo
mliitwa na nani, mimi siandiki kitu, niandike ili iweje, siwahitaji, kesi
imepangwa tarehe 28, pisheni wengine waendelee.
Naona kuna barua ya kumalizana katika nyumba ya maaskofu, kama ni hivyo
nawaombea usuluhishi mwema,”alisema Hakimu Simba.
Askofu
Mokiwa na wakili wake wote hawakufika mahakamani. Hata hivyo Wakili Masinga
alidai askofu huyo anataka kurejeshewa
uaskofu wake, anaomba mahakama itengue uamuzi wa kumstaafisha kwa nguvu.
“Mokiwa
alivuliwa uaskofu wake na Januari 7 mwaka huu akakimbilia mahakamani, mambo
yanayohusu imani yanatakiwa kushughulikiwa katika nyumba za imani.
“Huwezi
kuvuliwa madaraka msikitini ama kanisani ukakimbilia mahakamani, masuala hayo
yanajadiliwa katika vyombo husika labda pakiwapo ukiukwaji wa sheria za nchi,”alidai.
Kwa
mujibu wa barua kwa mapadri na maaskofu wote wa Kanisa la Anglikana Jimbo la
Dar es Salaam, kiongozi huyo alilazimishwa kuvuliwa uaskofu Januari 7 mwaka huu.
Sababu
za kuvuliwa madaraka kwa kiongozi huyo wa muda mrefu wa kanisa hilo ni kudaiwa
kuhusika na ufujaji wa mali za kanisa
na matumizi mabaya ya madaraka.
Inadaiwa
katika hati kwamba hatua hiyo inatokana na mashtaka yaliyowasilishwa dhidi yake
na wadhamini wa makanisa mbalimbali ya Jimbo la Dar es Salaam, ambayo ni Yombo
Buza na Magomeni ambao walilalamikia
matumizi mabaya ya madaraka kwa kile walichoita ufisadi huku wakimtaka
aandike barua mwenyewe ya kujiuzulu lakini aligoma kufanya hivyo.
Mokiwa
anakabiliwa na mashtaka 10 huku shtaka la tatu la uwekezaji, ndilo lililomtia
hatiani na yeye kukiri kosa mbele ya tume hiyo ya uchunguzi.
Kesi
hiyo itaendelea Februari 28 mwaka huu na
mahakama itaelezwa kama kuna makubaliano ya kuondoa kesi wakamalizane nje ya mahakama au la.
No comments