TRA YANASA MALI ZA MABILIONI DAR
MAMLAKA
ya Mapato Tanzania (TRA) imekamata bidhaa za magendo, zilizoingizwa nchini kwa
njia ya panya, ambazo zimeipotezea serikali kodi ya Sh bilioni 3.3 huku zikiwa
na thamani ya jumla ya Sh bilioni 4.
Aidha,
imetaja maeneo korofi yanayotumika kuingiza bidhaa hizo kuwa ni Bagamoyo,
Saadani, Mlingotini, Mbegani Juu, Mbweni, Ununio, Kunduchi, Kawe na Msasani.
Maeneo
mengine ni Kigamboni, Ufukwe wa Bamba, Kimbiji, Pemba Mnazi, Kibada, Nyamisati,
Kisiju, Mkuranga, Ubungo na katikati ya jiji.
Akitoa
taarifa hiyo Dar es Salaam juzi, Kaimu Mkurugenzi Elimu kwa Mlipakodi, Diana
Masala alisema kuwa bidhaa hizo, zimekamatwa maeneo mbalimbali ya jiji la Dar
es Salaam.
Zilikamatwa
katika msako uliofanywa na Jeshi la Polisi, Jeshi la Wananchi wa Tanzania
(JWTZ) na Idara ya Upelelezi Tanzania.
Alisema
kuwa bidhaa hizo zimekamatwa kwa kipindi cha kuanzia Januari hadi Desemba mwaka
huu kutokana na utaratibu wa kufanya doria na msako kwa pamoja katika maeneo ya
mwambao wa mikoa ya Dar es Salaam na Pwani.
“Bidhaa
zilizokamatwa ni majokofu yaliyotumika, luninga, simu za viganjani, kanga,
vitenge, chakula na mafuta ya kupikia. Kufanikiwa kukamatwa bidhaa hizi
kumetokana na ushirikiano kati ya TRA, Jeshi la Polisi, JWTZ, matumizi ya vifaa
vya kielekroniki na taarifa kutoka kwa wasamaria wema,” alisema Masala.
Alisisitiza
kuwa bidhaa za magendo, zinaathiri uchumi wa Taifa kwa ujumla na kwamba
wataendelea kudhibiti bidhaa za magendo kwa kufanya doria nchi kavu na
bandarini pamoja na misako ya kushtukiza katika maeneo hayo korofi.
Pia
aliongeza, watawatoza faini na kuwafutia leseni za biashara Mawakala wa Forodha
wanaojihusisha na vitendo viovu na kutoa semina kuhusu madhara na athari za
bidhaa hizo.
“Tunawaomba
wananchi wa maeneo hayo mtoe taarifa za shughuli za bidhaa bandia zinazofanywa
kwa kupiga simu namba 0789 338 930 itarahisisha ukamataji wa bidhaa hizo,”
aliongeza.
Katika
hatua nyingine, Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, imekusanya Sh
milioni 565.4 kupitia tozo mbalimbali za makosa ya usalama barabarani. Kamishna
wa Polisi Kanda hiyo, Simon Sirro alisema kuwa makusanyo hayo ni kwa kupindi
cha kuanzia Dsemba 22 mwaka huu hadi Desemba 30 mwaka huu.
‘’Idadi
ya magari yaliyokamatwa ni 17,645, bodaboda 1,406 na daladala 6,213 ambapo
jumla ya makosa yaliyokamatwa ni 18,849,’’ alisema Sirro.
Pia
aliwataka madereva hao kuwa makini kwa kuepuka ajali zisizo za lazima. Aliagiza
askari wa usalama barabarani kuhakikisha kuwa watakaobainika wanakiuka sheria
hizo wanachukuliwa hatua kali ikiwemo kupelekwa mahakamani na kutozwa faini.
|
No comments