TANESCO HALI BADO SI SHWARI, VIGOGO WENGINE KUTUMBULIWA, LENGO NI KUIMARISHA UTENDAJI WA SHIRIKA HILO
Siku
moja baada ya vigogo watatu wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kushushwa
vyeo, uongozi wa shirika hilo umesema utaendelea na fagio hilo kama njia ya
kuongeza ufanisi kwenye utendaji.
Vigogo
hao wa ngazi za juu ambao ni wakurugenzi, wamehamishiwa Chuo cha Mafunzo cha
Tanesco (TSS) kwa madai kuwa shirika linaboresha ufanisi wake.
Walioshushwa
vyeo ni pamoja na Declan Mhaiki aliyekuwa Naibu Mkurugenzi Mtendaji
anayeshughulikia usambazaji wa umeme.
Wengine
ni Naibu Mkurugenzi Mtendaji Uzalishaji na Huduma kwa Mteja, Mhandisi Sophia
Mgonja na Naibu Mkurugenzi Mtendaji Uzalishaji Umeme, Nazir Kachwamba.
Wakati
hao wakipitiwa na panga hilo, Mkurugenzi wa Idara ya Rasilimali Watu, Watson
Mwakyusa, aliamua kuandika barua kuacha kazi mwenyewe.
Juzi,
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Dk. Tito Mwinuka, alisema jana wangetoa
taarifa kuhusu hamisha hamisha hiyo.
Jana
mchana Idara ya Kitengo cha Mahusiano cha Shirika hilo, kilitoa taarifa na kusema
kuwa wataendelea na hatua mbalimbali za mabadiliko ya uongozi kwa lengo la
kuongeza ufanisi zaidi wa kiutendaji.
Taarifa
hiyo ilieleza kuwa mabadiliko yanayoendelea ndani ya Tanesco yatawekwa wazi
wakati mwafaka kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu za shirika kupitia
vyombo vya habari.
Kitengo
hicho kilieleza kuwa kwa sasa bado wanaendelea na panga pangua na endapo
watakamilisha watatoa taarifa kwa umma.
“Tunaomba
vyombo vya habari vitoe fursa kwa mamlaka husika kuendelea kukamilisha zoezi
hili muhimu kwa maendeleo ya Shirika na Taifa kwa ujumla na taarifa rasmi
itatolewa baada ya zoezi kukamilika,’’ ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.
Januari
Mosi, mwaka huu, Rais Dk. John Magufuli alimteua Dk. Mwinuka kuwa Kaimu
Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, baada ya kumng’oa aliyekuwa mkurugenzi wa
shirika hilo, Mhandisi Felchesmi Mramba.
Mramba
alitenguliwa uteuzi wake siku mbili baada ya Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za
Nishati na Maji (Ewura), kutangaza kuridhia ombi la Tanesco la kupandisha bei
ya umeme kwa asilimia 8.5 kutoka 18 waliyoomba.
Kabla
ya uteuzi huo, Dk. Mwinuka alikuwa Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam
(UDSM).
Akiwa
mjini Bukoba kwenye ibada ya Mwaka Mpya, Rais Magufuli alisema amekerwa na
kusikitishwa na vitendo vya baadhi ya watumishi wa umma kujitokeza hadharani na
kutangaza au kuzungumzia mambo ya kitaifa kama uamuzi wa Serikali bila
kushirikisha viongozi wao wa ngazi za juu.
Kutokana
na hali hiyo, alisema watendaji hao ni miongoni mwa majipu yanayostahili
kutumbuliwa.
No comments