SAKATA LA ASKOFU MOKIWA KUTUMBULIWA DAR MAPYA YAIBUKA
KATIBU
Mkuu Kanisa la Anglikana Tanzania, Johnson Chinyong’ole amesema aliyekuwa
Askofu wa Dayosisi ya Dar es Salaam, Dk Valentine Mokiwa anakabiliwa na
mashitaka ya jinai kwa kuingia mikatiba mibovu na matumizi mabaya ya fedha za
kanisa makosa yanayoangukia kuvunja sheria za nchi.
“Hatujakurupuka
kuchukua hatua, ushahidi wote tumeshauwasilisha kwa vyombo vinavyohusika
serikalini, sisi tumetimiza wajibu wetu, hivyo tunaviachia vyombo vinavyohusika
kufanya kazi yake katika eneo hilo la ubadhirifu wa fedha,” alisema
Chinyong’ole.
Alifafanua
kuwa wakati wanaenda kutangaza uamuzi wa kumvua uaskofu Dk Mokiwa juzi kanisa
la Ilala, walienda kutoa taarifa kwa msajili wa vyama ambaye ndiye anayesajili
makanisa, lakini pia wameshatoa taarifa katika ofisi za Wakala wa Usajili,
Ufilisi na Udhamini (RITA) kwa ajili ya kuchukua hatua za kisheria.
Alitaja
sheria alizovunja Dk Mokiwa kuwa ni sheria ya miunganiko ya wadhamini sura ya
318, sheria ya ardhi namba 4 ya 1999 na sheria ya mipango miji sura ya 355 kwa
kuruhusu mabadiliko ya matumizi ya ardhi katika shamba la kanisa la Mtoni Buza
na eneo la Kanisa la Mtakatifu Mariam Kurasini.
“Sisi
tunasubiri mrejesho kutoka ofisi ya Waziri Mkuu, Rita na kwa Msajili wa vyama
vya kiraia,” alisema katibu mkuu huyo wa kanisa la Anglikana Tanzania.
Alifafanua
kuwa katika mashitaka 10 anayokabiliwa nayo, shitaka la tatu ndilo ambalo ni la
ubadhirifu wa mali za kanisa ndilo ambalo linaifanya serikali kuingilia kati.
Alisema
makosa ya Dk Mokiwa yanahusisha pia kughushi na akatoa mfano wa kuingia
mikataba kwa kuwatumia watu ambao si wadhamini wa kanisa hilo wakati sheria
inamtaka atumie wadhamini wawili wanaosimamia mali za kanisa, pamoja na
kutumika kwa muhuri bandia wakati sheria inasisitiza muhuri unaotumika ni ule
wa moto.
Katibu
Mkuu huyo alisema ripoti ya tume iliyoundwa kuchunguza tuhuma dhidi ya askofu
hiyo yenye kurasaa 173 imewasilishwa pia serikalini ili vyombo vinavyohusika
kufuatilia tuhuma hizo viweze kujiridhisha wakati vinapoenda kuchukua hatua.
“Hakuna
mtua aliyeonewa, wala kuchafuliwa, hizi ni tuhuma za ubadhirifu wa mali ya
kanisa, lazima vyombo vya dola vihusike hapa,” alisema katibu mkuu huyo na
kuongeza kuwa serikali ndio inayotakiwa kuchukua hatua kwa sababu tume
iliyoundwa na kanisa imeshaweka hadharani ushahidi kwa lengo la kuokoa mali za
kanisa.
Amevunja
kiapo cha utii Kwa hali hiyo jambo hilo tayari wameliwasilisha kwa msajili wa
vyama ambaye ndiye msajili wa kanisa hilo na pia wamewasilisha suala hilo kwa
wakala wa vizazi na vifo (Rita) kwa kuwa sheria ya nchi iliyovunjwa ni ya
udhamini.
Akizungumza
na gazeti hili jana, Chinyong’ole alisema kwa mujibu wa katiba ya kanisa hiyo
ya mwaka 1970 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2004, pamoja na Dk Mokiwa kugoma
kung’oka madarakani baada ya kuvuliwa madaraka yake na askofu mkuu Dk Jacob
Chimeledya, kwa sasa katiba haimtambui kama askofu wa kanisa hilo.
Alisema
kabla ya marekebisho ya mwaka 2004, sinodi ya dayosisi ndio ilikuwa inakuwa na
tamko la mwisho dhidi ya askofu wa dayosisi, lakini baada ya marekebisho
kufanyika askofu mkuu ndiye msimamizi wa maaskofu wote wa dayosisi na ana
mamlaka ya kuwastaafisha pale wanapokiuka katiba ya kanisa.
“Dk
Mokiwa amenyang’anywa utawala wa dayosisi ya Dar es Salaam, katiba inampa
mamlaka askofu mkuu kuwastaafisha maaskofu ikibainika wameenda kinyume cha
sheria na katiba ya kanisa,” alisema Chinyong’ole.
Aliongeza
kuwa baada ya kumvua utawala wa dayosisi, hatua inayofuata ni taratibu zingine
za kisheria ambazo zitashughulikiwa na kanisa ikiwa ni pamoja na kumbana Dk
Mokiwa kukiuka kiapo chake cha kumtii askofu mkuu wa kanisa.
Alisisitiza
kuwa Dk Mokiwa amevunja kifungu namba 7 cha katiba ya kanisa hilo kuhusu kiapo
cha utii kwa askofu mkuu aliposema
“Nakubali
na kuahidi kumheshimu na kumtii, kama inipasavyo, askofu mkuu wa kanisa
Anglikana Tanzania... watakaofuata baada yake...”
Katibu
mkuu huyo alisema Dk Mokiwa kutokana na hatua yake kugoma kujiuzulu baada ya
kushauriwa na askofu mkuu Tanzania, amevunja kiapo cha utii kwa katiba ya jimbo
kinachosema,
“Ninaahidi
pia kwamba nitakubali kujiuzulu au kujitoa kwa hukumu yoyote itakaoniachisha
madaraka na mapato yanayohusika na dayosisi hii nitakayohukumiwa wakati wowote
baada ya uchunguzi wa kutosha wa barza lenye kbali cha sinodi ya kanisa.”
Pia
amevunja kiapo cha utii kwa katiba ya dayosisi kinachosema “Ninaahidi pia
kwamba nijiuzulu wakati wowote kama ikiazimiwa na Askofu Mkuu wa Kanisa
Anglikana Tanzania kwa mujibu wa katiba ya kanisa na ya Dayosisi.”
Wachunguzi
wa mambo wanabainisha kuwa kugoma kwa Dk Mokiwa kung’oka madarakani kutaleta
mtafaruku mkubwa ndani kanisa hilo kutokana na baadhi ya makanisa katika
Dayosisi ya Dar es Salaam kuunga mkono uamuzi wa askofu mkuu na wengine
wanamuunga mkono Dk Mokiwa.
Juzi,
Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Dk Jacob Chimeledya alimvua
uaskofu mkuu wa Dayosisi ya Dar es Salaam, Dk Mokiwa baada ya mashitaka 10
yaliyofunguliwa na walei 32 wa kanisa hilo katika dayosisi hiyo kumtuhumu kwa
ufisadi wa mali za kanisa hilo.
Uamuzi
huo ulichukuliwa baada ya Askofu Mokiwa kugoma kujiuzulu kama ilivyoshauri
nyumba ya maaskofu ambayo ilimkuta na hatia ya ufujaji wa mali za kanisa hilo
na kukiuka maadili ya kiuchungaji ambayo yalibainishwa kwenye ripoti ya
uchunguzi ya kanis ahilo nchini.
Hata
hivyo, Dk Mokiwa amegomea uamuzi huo kwa maelezo kuwa, mwajiri wake ni Sinodi
ya Dar es Salaam ambayo ndio yenye uamuzi wa kumfuta kazi na si askofu mkuu au
askofu mwingine yeyote wa kanisa la Anglikana Tanzania.
Chanzo-Habarileo
No comments