ILE KESI YA MAPACHA WA KIARABU KUTISHIA KUUA WAANDISHI SINGIDA KUUNGURUMA JANUARI 16
PACHA
wenye asili ya kiarabu wanaoshitakiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi mjini
Singida kwa kutishia kuua waandishi wa habari mkoani Singida, watasomewa
maelezo ya awali Januari 16.
Pacha
hao ambao ni wafanyabiashara maarufu mjini hapa, kwa mara ya kwanza,
walifikishwa mahakama hapo, Novemba 18 mwaka jana. Washitakiwa hao, Hassan
Salehe na Hussein Salehe (47) ni wakazi wa eneo la mji wa zamani katika kata ya
Mughanga, Manispaa ya Singida.
Ilidaiwa
na Mwanasheria wa Serikali, Ahmed Seif kuwa washitakiwa kwa pamoja walitenda
kosa hilo Novemba 07, mwaka jana saa 3:00 asubuhi katika Ofisi za Klabu ya
Waandishi wa Habari Mkoa wa Singida (Singpress) zilizopo eneo la Msufini mjini
Singida.
Mbele
ya Hakimu wa mahakama hiyo, Terrisophia Tesha, Seif alidai kuwa siku ya tukio
washitakiwa walikwenda kwenye ofisi hizo na kutoa maneno ya kutishia kuwaua
waandishi wa habari wanaoandika habari kuhusiana na tuhuma inayowakabili kwenye
kituo cha polisi.
Awali,
watuhumiwa hao walifikishwa Polisi kwa tuhuma za kumpiga binti yao waliyedai
ana uhusiano wa kimapenzi na kijana 'mswahili' na kuchukua mali yote ya kijana
huyo wakidai ameipata kutokana na kuhongwa na binti yao.
Baada
ya vyombo vya habari kutangaza taarifa hizo, ndipo pacha hao walipoamua kwenda
ofisi za Singpress na kutoa tishio hilo.
Washitakiwa
walikana shitaka na wapo nje kwa dhamana.
ABBY
NKUNGU-HABARILEO SINGIDA
No comments