MARC NA MADC MSIOGOPE KUTUMBULIWA, SEMENI UKWELI KUHUSU BAA LA NJAA: MGEJA
WAKUU
wa mikoa na wakuu wa wilaya nchini wametakiwa kujitokeza hadharani kutoa tamko
rasmi la baa la njaa linalowakabili wananchi kwenye maeneo yao wanayoyaongoza.
Mwenyekiti
wa Tanzania Mzalendo Foundation Khamis Mgeja alisema hayo wakati akiongea na
waandishi wa habari alipokuwa anatoa salamu za mwaka mpya akiwa mkoani Tabora
kwa mapumziko ya sikukuu ya mwaka mpya 2017.
Mgeja
alisema anawaomba kwa heshima wasiogope kusema ukweli kwa woga wa kutumbuliwa
na mamlaka za juu zilizowateua kwani hali ya baa la njaa nchini ni kubwa katika
baadhi ya maeneo mbalimbali nchini.
Alisema
inasikitisha kuona baadhi ya viongozi wakikaa kimya na ukimya huo unawaumiza
wananchi huku viongozi hao wakifumbia macho jambo hili eti kwa hofu ya
kutumbuliwa.
Alisema
ni lazima wakuu wa mikoa na wa wilaya watambue cheo ni dhamana na hakuna mtu
aliyezaliwa na uongozi bali watambue uongozi ni matokeo tu yanayomkuta
mwanadamu katika mchakato wa maisha yake.
Aidha
alisema uongozi siyo jambo la kudumu na
na nje ya ukuu wa mkoa na wilaya
kuna maisha hivyo kutokana na baa la njaa lililopo kwenye baadhi ya
maeneo, wakuu wa wilaya na mikoa wakubali kuwa kafara na kujitoa sadaka kwa
ajili ya wananchi kwa kujitokeza kusema ukweli.
Mgeja
alisema tatizo lililopo la njaa kwenye baadhi ya maeneo
linapelekea
baadhi ya wananchi kulalia uji na wengine maembe na hili ni janga kubwa kwa
taifa.
Alisema
hakuna aibu wala kosa kusema ukweli lakini tatizo lililopo la nchi yetu umezuka
ugonjwa mbaya sana wa uoga na hofu kwa viongozi na watendaji baadhi kwa sasa
wana hofu na uoga wa kiutendaji wakihofia kutumbuliwa.
Mgeja
alisema faida ya kusema ukweli itasaidia serikali kujipanga vizuri hivyo
kuiomba serikali pia iwe sikivu kwa suala la njaa linalokabili wananchi na
kwamba ni lazima viongozi wawe wanawapa wananchi maneno ya matumaini kuliko
kuwakatisha tamaa.
Alisema
serikali kuwaaeleza wananchi kuwa ‘serikali haina shamba wala chakula cha bure’
au ‘mwafaa’ maneno hayo hayaleti afya wala matumaini kwa wananchi
wanaowaongoza.
Alimshauri
waziri mkuu Kassim Majaliwa kwamba kuanzia sasa katika ziara zake anapotembelea
miradi mbalimbali katika wilaya na mikoa hasa iliyokumbwa na baa la njaa basi
atembelee na shehena ya chakula cha njaa.
Mgeja
alimuomba Waziri Mkuu pia awe anatanguliza chakula cha njaa sehemu anazokwenda
kwani kitengo cha maafa kiko chini yake na wapo wananchi wanaohitaji chakula
cha bure na wapo wanaohitaji kuhudumiwa.
Alisema
wapo pia wanaojiweza lakini uwezo wao ni mdogo wa kumudu bei za sokoni zilizopo
sasa na kama chakula cha serikali kikiwafikia bei yake itakuwa chini na watu
kipato cha chini watamudu kununua chakula hicho.
Mgeja
aliiomba na kuishauri serikali kulipa kipaumbele suala hilo na hasa katika
kilimo cha mwaka huu mazao yameanza kunyauka kutokana na ukame mkubwa kutokana
na mvua kutonyesha vya kutosha.
Aliishauri
na kuiomba serikali ya awamu ya tano iweke wazi juu ya akiba ya chakula kuwa
kuna kiasi gani ili wananchi wajue kwani ni haki yao kwa sababu chakula ni cha
umma na wana haki kujua.
"Serikali
inaposhindwa kusema ukweli kuhusu baa la njaa eti kwa sababu ya kiusalama wa
kitaifa sasa tunajiuliza je chakula nacho kimekuwa zana za ‘Kivita’?, ni vyema
serikali ikawa wazi kuhusiana na akiba ya chakula ili wananchi wapate fursa ya
kujipanga vizuri kwa kujifunga mkanda",aliongeza Mgeja.
No comments