KUFATIA KUSAMBAA VIDEO KATIKA MITANDAO YA KIJAMII WAKIMCHAPA MWANAMKE VIBOKO 30, WATU 10 MBARONI RORYA
JESHI la Polisi Kanda Maalumu
ya Tarime/Rorya mkoani Mara, linawashikilia watu 10 kwa udhalilishaji wa
kumchapa viboko mwanamke hadharani.
Watu hao ni wa kijiji cha Kinesi
tarafa ya Suba wilayani Rorya. Miongoni mwa watu hao, wamo viongozi watano wa
baraza la mila liitwalo Irienyi ndogo la kabila la Wasimbiti.
Watu hao wanatuhumiwa kumchapa
viboko zaidi ya 30 hadharani mwanamke huyo, kitendo kilichomdhalilisha mbele ya
jamii.
Mapema wiki hii, baadhi ya
video ilisambaa katika mitandao ya kijamii, ikimuonesha mwanamke akichapwa
viboko na wanaume kwa zamu huku akilia mbele ya hadhara na sauti za wanaume
zilisikika zikishabikia kitendo hicho.
Kamanda wa Polisi Tarime/ Rorya,
Andrew Satta alisema kuwa tukio hilo ni la Desemba 23 mwaka jana mchana katika
kitongoji cha Migutu kijiji cha Kinesi tarafa hiyo ya Suba wilayani Rorya
katika maeneo ya Mastooni, ambako kulikuwa na mkutano wa Ritongo wa mila.
Mwanamke huyo mwenye umri wa
miaka 38, mkazi wa kijiji hicho (jina limehifadhiwa) aliitwa na kufuatwa na
vijana na kupelekwa katika mkutano huo wa mila, uliohudhuriwa na mamia ya
wakazi wa kijiji hicho. Ilidaiwa kuwa mwanamke huyo alimtuhumu mama yake mzazi
wa umri wa miaka 55 kuwa ni mchawi.
Kwamba hamtambui na kumkana
kuwa si mama yake mzazi; huku akidai kuwa mama huyo anataka kumuua kwa uchawi.
Kamanda Satta alisema katika
mkutano huo wa baraza la mila la Irienyi, vijana sita waliamriwa kumchapa kila mmoja
viboko vitano makalioni mwanamke huyo, hali iliyomsababishia majeraha,
kumuathiri, kumdhalilisha na kumshushia utu wake kwa jamii.
“Tumewakamata mwenyekiti wa
baraza hilo, viongozi wenzake wanne na vijana sita walioshiriki kumkamata na
kuadhibu kwa kumlaza chini, kumchapa viboko na kumsababishia madhara makubwa
mwilini na kumdhalilisha,” alisema Kamanda. Alisema watuhumiwa hao wanahojiwa
na jeshi hilo linaendelea kuwasaka wengine waliohusika.
No comments