KAULI YA TUME YA UCHAGUZI KUHUSU MALALAMIKO YA UKIUKWAJI WA MAADILI YA UCHAGUZI YALIYOTOLEWA NA CHAMA CHA ACT WAZALENDO
Tume
ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imekishauri Chama cha ACT – Wazalendo na Vyama
vingine vyenye wagombea wa Ubunge katika Uchaguzi Mdogo wa Jimbo la Dimani na
Udiwani katika Kata Ishirini (20) za Tanzania Bara ,kuwasilisha malalamiko ya
ukiukwaji wa Maadili ya Uchaguzi kwenye Kamati za Maadili zilizo katika maeneo
yao.
Akizungumza
na vyombo vya habari leo jijini Dar es salaam, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya
Taifa ya Uchaguzi (NEC), Bw. Kailima Ramadhan amesema NEC imepata taarifa
kupitia Vyombo mbalimbali juu ya malalamiko ya Chama Cha ACT-Wazalendo
kuvilalamikia Vyombo vya Dola pamoja na Watendaji wa Umma kufanya vitendo
vyenye muelekeo wa kukipendelea Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Bw.
Kailima amesema taarifa ya Chama hicho iliyotolewa kwenye Vyombo vya Habari
Januari, 12 2017, imeeleza kuwa Watendaji wa Halmashauri ya Geita waliwakusanya
Wazee katika Kata ya Nkoma waje na Vitambulisho vyao vya kupigia Kura kwa lengo
la kuwapatia huduma ya afya bure jambo linalolalamikiwa na ACT- Wazalendo kwa
madai kwamba Watendaji hao wana lengo la kuwahadaa Wazee hao ili wakipigie Kura
Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Aidha,
amesema katika malalamiko yake Chama cha ACT Wazalendo kimeibua tuhuma za
wananchi kupokwa kadi za kupigia Kura ili wasiweze kushiriki katika uchaguzi
mdogo utakaofanyika Januari 22, 2017.
Mkurugenzi
Kailima amesisitiza kuwa ni kosa chini ya kifungu cha 88 cha Sheria ya Taifa ya
Uchaguzi, Sura ya 343 na kifungu cha 100 cha Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za
Mitaa, Sura ya 292 mtu kumiliki kadi ya kupigia kura isiyokuwa yake.
“Natoa
wito kwa wananchi wote kwamba, ni kosa chini ya kifungu cha 88 cha Sheria ya
Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343 na kifungu cha 100 cha Sheria ya Uchaguzi ya
Serikali za Mitaa, Sura ya 292 mtu yeyote kumiliki kadi ya kupigia kura
isiyokuwa yake” Amesema.
Amefafanua
kuwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa kuzingatia sehemu ya 5.4 ya Maadili ya
Uchaguzi inavikumbusha Vyama vya Siasa kuwa iwapo vitakuwa na malalamiko ya
ukiukwaji wa Maadili ya Uchaguzi katika Uchaguzi Mdogo wa Udiwani viwasilishe
malalamiko hayo kwenye Kamati ya Maadili ngazi ya Kata ndani ya saa 72 tangu
kutokea kwa tukio linalolalamikiwa.
“
Sehemu ya 5.4 ya Maadili ya Uchaguzi yayosainiwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi,
Serikali na Vyama Vya Siasa inaeleza wazi muda wa kuwasilisha malalamiko kwa
kuvitaka vyama au wahusika wenye malalamiko yoyote kuyawasilisha kwa maandishi
kwenye Kamati ya Maadili ya Uchaguzi ya ngazi husika ndani ya saa 72 tangu
kutokea kwa tukio” Amesisitiza Kailima.
Amesisitiza
kuwa iwapo Chama cha Siasa au Mgombea hataridhika na maamuzi ya Kamati ya
Maadili ngazi ya Kata, kwa kuzingatia sehemu ya 5.7 (a) ya Maadili ya Uchaguzi
anatakiwa awasilishe rufaa yake kwa Msimamzi wa Uchaguzi ngazi ya Jimbo ndani
ya saa 24 tangu maamuzi ya Kamati ya Maadili ngazi ya kata kutolewa.
Aidha,
Bw. Kailima amebainisha kuwa kama Chama cha Siasa hakikuridhika na maamuzi ya
Kamati ya Maadili ngazi ya Jimbo, bado kwa kuzingatia sehemu ya 5.7 (b) na (c)
kinayo fursa ya kuwasilisha Rufaa yake katika Kamati ya Maadili ngazi ya Taifa
au ngazi ya Rufaa ambayo ni Tume ya Taifa ya Uchaguzi.
“
Tunavishauri Vyama vya Siasa na Wagombea kuzingatia matakwa ya Maadili ya
Uchaguzi katika kuwasilisha malalamiko yao ya ukiukwaji wa maadili ya Uchaguzi,
kwa mujibu wa sehemu ya 5.7(e) ya Maadili ya Uchaguzi, pale ambapo Chama cha
Siasa au Mgombea hakuridhika na maamuzi ya Kamati ya Rufaa atakuwa na fursa ya
kuwasilisha malamiko yake Mahakamani baada ya Uchaguzi kwa mujibu wa Sheria ya
Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343 na Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa, Sura
ya 292”.
Amesisitiza
kuwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi inaendelea kuwasihi viongozi wa Vyama vya Siasa
na Wadau wengine wa Uchaguzi kuendelea na Kampeni za kistaarabu na kuzingatia
Sheria, Kanuni na Maadili ya Uchaguzi na kwamba inaendelea kufuatilia kwa
karibu kila hatua ya Uchaguzi na hasa Kampeni huku akisisitiza kuwa haitasita
kuchukua hatua kwa mtu yeyote atakayekiuka Sheria za Uchaguzi.
No comments