HATIMAYE NJIA YA RELI KATI YA DAR ES SALAAM NA RUVU YAFUNGULIWA
Uongozi
wa Kampuni ya Reli Tanzania (TRL) umetoa taarifa kuwa kuanzia saa 9 alasiri leo
Januari 30, 2017 njia ya reli kati ya Kituo Kikuu cha Dar es salaam na Ruvu
imefunguliwa rasmi kwa shughuli za uendeshaji wa reli.
Taarifa hiyo imesema kuwa kazi ya ufunguaji njia
imewezekana baada ya Wahandisi na Mafundi wa reli kuyaondoa Mabehewa yaliopata
ajali kutoka relini na pia kuikarabati sehemu iliyoharibika . Kazi hiyo
imefanyika kuanzia usiku wa Januari 29, 2017 hadi mchana wa Januari 30, 2017.
Aidha treni ya abiria iliyoahirisha safari ya
kuondoka kwenda bara jana imeondoka leo saa 9:05 alasiri kutoka kituo kikuu cha
Dar es Salaam kwenda bara..
Wakati huo huo imefahamika kuwa msafiri mmoja
aliyetambulikana kama Nd Basekena O. Bango kutoka Bujumbura Burundi akiwa
anasafiri kutoka Kigoma amelazwa katika Hospitali ya Tumbi Kibaha mkoani wa
Pwani kwa ajili ya matibabu zaidi. Aligunduliwa kuwa amechanika mguu wake wa
kulia hivyo basi kuhitaji kushonwa mguu wake huo.
Taarifa kutoka Muhimbili zinaeleza kulazwa kwa
majeruhi wawili waliopokelewa hospitalini hapo usiku wa Januari 29, 2017.
Majeruhi wamefahamika kuwa ni Nd. Stephania Mbona (46) kutoka Kigoma alikuwa
amekuja Muhimbili kuendelea na matibabu ya ugonjwa wa tumbo, hata hivyo
alitibiwa majeraha ya kawaida na anaendelea kulazwa kwa ajili ya matibabu ya
ugonjwa wake wa tumbo.
Mgonjwa wa pili Nd Alice Jovin (37) mkazi wa
Salasala Dar es Salaam alikuwa anatoka Kigoma kuja Dar es Salaam amepata
majeraha ya kawadia ametibiwa na alitarajiwa kuruhusiwa leo asubuhi.
Kuhusu idadi ya wasafiri treni ya Deluxe yenye
uwezo wa kusafirisha abiria zaidi ya 1000 wakati inapata ajali ilikuwa na abiria
480.
Aidha imefahamika kuwa ili kufahamika hasara na
sababu za ajali hiyo taarifa rasmi itatolewa baada ya uchunguzi wa Kamati
maalum inayoundwa kwa mujibu wa sheria, taratibu na kanuni za uendeshaji reli
za kimataifa. Taarifa hiyo itatolewa baada ya wiki mbili.
Imetolewa na Afisi ya Uhusiano:
Kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa TRL
Ndugu Masanja Kungu Kadogosa
Januari 30, 2017
DAR ES SALAAM
No comments