WASSIRA ATINGA MAHAKAMA YA RUFAA KUMPINGA BULAYA
WAZIRI
mwandamizi wa serikali ya Tanzania kwa awamu nne za uongozi, Stephen Masato
Wassira, kupitia kwa wafuasi wake watatu, amekata rufaa Mahakama ya Rufaa,
akipinga uamuzi wa Mahakama Kuu kwa kuhalalisha ushindi wa Mbunge wa Bunda
Mjini, Esther Bulaya (Chadema).
Wassira
(71 ) alikuwa waziri kwa mara ya kwanza tangu Desemba 07, 1973 akiwa naibu
waziri wa Kilimo na ameendelea kuwa kiongozi mwandamizi wakati wa serikali ya
Mwalimu Julius Nyerere, akarithiwa wakati wa Rais Ali Hassan Mwinyi, baadaye
Rais Benjamin Mkapa na hatimaye uongozi wa awamu ya nne wa Rais Jakaya Kikwete.
Tayari
wafuasi hao wa Wassira; Magambo Masato, Matwiga Matwiga na Ascetic Malagaila,
wamefungua kesi hiyo na imesajiliwa katika ofisi za mahakama ya rufaa jijini
Mwanza tarehe 16 Desemba, 2016 na itakuwa ni kesi ya rufaa namba 199 ya mwaka
2016.
Katika
rufaa hiyo iliyoandikwa na wakili wao, Constatine Mutalemwa, wametoa sababu
kadhaa kama hoja zao za kukata rufaa.
Kwanza,
wanadai kwamba jaji hakuzingatia makosa yaliyofanyika baada ya zoezi la kupiga
kura.
Pili,
Wassira au wakala wake wanadai hakuitwa kwenye majumuisho kujulishwa siku,
mahali wanafanyia majumuisho.
Tatu,
wanadai kuwa jaji hakutilia maanani kesi zinazofanana na hii zilizotolewa kama
mfano mahakamani.
Nne,
Jaji alikosea kutoa uamuzi kwa misingi ya maoni binafsi badala ya kuzingatia
mambo ya maana.
Wanadai
kuwa jaji alisema wananchi wa Bunda ni maskini waachwe wafanye shughuli za
maendeleo kwa sasa.
Tano,
wanadai jaji alikosea kuamua kuhusu sheria ya viapo na matamko iliyotajwa
katika kanuni za kuendesha kesi za uchaguzi.
Novemba
18, mwaka huu, Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza ilitoa uamuzi wa kesi ya kupinga
matokeo ya uchaguzi wa ubunge uliompa ushindi Mbunge wa Bunda Mjini, Esther
Bulaya (Chadema) dhidi ya Stephen Wassira (CCM).
Kesi
hiyo ya kupinga matokeo ya uchaguzi ilifunguliwa katika Mahakama Kuu Kanda ya
Mwanza, lakini ilikuwa inasikilizwa mjini Musoma, mkoani Mara.
Mahakama
hiyo ilieleza kutoridhishwa na ushahidi wa kupinga matokeo hayo uliowasilishwa
na upande wa walalamikaji, hivyo ikamthibitisha Bulaya kuwa mbunge halali wa
jimbo hilo.
Kesi
ya kupinga matokeo hayo ilifunguliwa na wafuasi wa Wassira ambaye alikuwa
mbunge wa jimbo hilo kabla ya kuondolewa kupitia uchaguzi mkuu uliofanyika
mwaka jana.
Katika
kesi ya msingi, walalamikaji ambao ni wakazi wa Bunda walidai kuwa uchaguzi
haukuwa huru na haki kwakuwa uligubikwa na vitendo vya rushwa, mgombea
wanaemuunga mkono kunyimwa fursa ya kuhakiki matokeo pamoja na kuongezeka kwa
idadi ya vituo vya kupigia kura visivyo halali.
Katika
kesi hiyo, Bulaya alitetewa na mwanasheria wa Chadema, Tundu Lissu.
Credit:
FikraPevu
No comments