PROF MBARAWA:KAMPUNI MAWASILIANO NCHI KUSAJILIWA SOKO LA HISA.
Waziri
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa, amezitaka Kampuni za
Mawasiliano kukamilisha taratibu za usajili katika Soko la Hisa la Dar es
Salaam kwa kuuza asilimia 25 ya hisa zote kadri ya Sheria ya Masoko ya Mitaji
na Dhamana inavyoelekeza mwishoni mwa mwaka huu.
Akizungumza
jijini Dar es Salaam, Prof. Mbarawa ametaja kampuni hizo kuwa ni zile zenye
leseni za mawasiliano zilizotolewa kabla ya tarehe 1 Julai 2016 kwa ajili ya
Miundombinu ya Mawasiliano, Huduma za Mawasiliano, na Huduma za Matumizi.
“Watoa
huduma wote wa Mawasiliano wajisajili na kuuza hisa zao kwa wananchi ndani ya
mwezi wa Disemba”, amesema Waziri Prof. Mbarawa.
Ameongeza
kuwa kwa Kampuni zilizopata leseni baada ya tarehe mosi Julai, 2016 watatakiwa
kutimiza sharti hilo la kisheria kwa kipindi kisichozidi miaka miwili tangu
kusajiliwa.
Waziri
Prof. Mbarawa amesisitiza kuwa Kampuni zitakazokiuka Sheria hiyo zitachukuliwa
hatua za kisheria kupitia kifungu cha 21 (C) cha EPOCA, 2010.
Aidha,
amewataka wananchi kutumia fursa hiyo kununua hisa hizo na kuwa sehemu ya
wamiliki wa makampuni ya Mawasiliano ili kuongeza kipato na kushiriki katika
maamuzi ya kampuni hizo.
No comments