TUME YA UCHAGUZI ATANGAZA RATIBA YA KAMPENI ZA UCHAGUZI MDOGO WA UBUNGE NA UDIWANI
Mwenyekiti mpya wa Tume ya
Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji Semistocles Kaijage, ametangaza ratiba ya kuanza
kwa kampeni za uchaguzi mdogo wa ubunge wa Jimbo la Dimani, lililopo Zanzibar
na mwingine wa nafasi za udiwani katika Halmashauri za Manispaa 20 zilizoko
Tanzania Bara.
Jaji Kaijage alitangaza ratiba
hiyo katika ofisi za NEC, ikiwa ni siku moja tu baada ya Rais Dk. John Magufuli
kumteua zi na kumuapisha Ikulu, Dar es Salaam jana.
Duru za siasa zinadai kuwa
hatua ya Jaji Kaijage kutangaza ratiba ya kampeni hizo zinazoonyesha kuanza
jana Desemba 23, mwaka huu hadi Januari 21, mwakani ni fursa kwa vyama vya
siasa, hasa vya upinzani vilivyosimamisha wagombea wa uchaguzi huo kuanza
kufanya mikutano ya hadhara iliyopigwa marufuku hadi mwaka 2020.
Mikutano ya hadhara ya vyama
vya siasa ilipigwa marufuku Juni, mwaka huu na Magufuli, kwa kile alichokisema
kuwa muda wa kufanya siasa umeshamalizika kwa kuwa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25,
mwaka jana umekwisha na viongozi waachwe wafanye kazi za kuwatumikia wananchi.
Hata hivyo, agizo hilo
lilipingwa na Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema),
Freeman Mbowe, aliyemtaka Magufuli ajiandae kwa lolote, ikiwamo kuongeza
magereza baada ya kuvikataza vyama vya siasa kufanya shughuli za kisiasa hadi
baada ya miaka mitano ijayo, lakini baadaye Jeshi la Polisi likaviruhusu vyama
vya siasa kufanya mikutano ya ndani na si ya hadhara.
Duru hizo zinaendelea kudai
kuwa, kitendo cha mikutano ya hadhara kuzuiliwa kwa miaka mitano na hatua ya
kuanza kwa kampeni hizo zilizotangazwa na Jaji Kaijage pengine itatoa nafasi
kwa vyama vya siasa kujipanga na kuwatumia viongozi wao wa kitaifa kufanya
kampeni Dimani na katika kata 20 na kutumia mikutano hiyo kukosoa mwenendo wa
Serikali ya Magufuli.
Pia duru hizo zinasema kuwa,
uchaguzi mdogo utakuwa wa aina yake kama vyama vya upinzani vitawatumia
viongozi wao wa kitaifa katika kampeni hizo.
Lakini Jaji Kaijage amevitaka
vyama vya siasa na wagombea wake kufanya kampeni za kistaarabu ili kufanikisha
uchaguzi huo wa marudio utakaofanyika Januari 22, mwakani.
“Kwa mujibu wa kanuni za
maadili, kampeni zinatakiwa kuwa za kistaarabu na zinapaswa kuanza saa mbili
asubuhi hadi saa 12 jioni. Kamati za maadili zinaundwa katika ngazi mbalimbali
ambapo zitakuwa na jukumu la kusimamia utekelezaji wa maadili katika kipindi
chote cha kampeni,” alisema Jaji Kaijage.
Pia alisema pale penye
malalamiko, kamati hizo zitatoa uamuzi ili kuweka usawa katika uwanja wa
kampeni.
“Vyama vya siasa vinakumbushwa
kuzingatia maadili na ratiba za kampeni katika maeneo husika kwa mujibu wa
ratiba iliyoratibiwa na msimamizi wa uchaguzi.
“Ratiba hii ilikubaliwa na
vyama vinavyoshiriki uchaguzi na kwa mujibu wa sheria iliwasilishwa kwa
msimamizi wa uchaguzi siku saba kabla ya uchaguzi na pale penye malalamiko
chama husika kitapaswa kuwasiliana na msimamizi wa uchaguzi ili aviarifu vyama
vingine,” alisema.
Pia alisema vyama vya siasa 13
vinatarajiwa kuchuana kugombea nafasi za udiwani katika kata hizo 20, huku
vingine 11 vikichuana kugombea ubunge wa Dimani.
Alisema jumla ya wagombea wote
ni 83, huku 11 wakiwa ni wa ubunge na wagombea wa nafasi ya udiwani wakiwa ni
72 na kati yao, watano ni wanawake.
“Kwa mujibu wa kifungu cha
37(1) b cha sheria ya Uchaguzi, sura ya 343 na kifungu cha 41(1) vya sheria ya
uchaguzi wa Serikali za Mitaa, sura ya 292 Tume imefanya uteuzi kwa wagombea wa
ubunge na udiwani kwa kata mbalimbali. Jumla ya vyama 11 vimesimamisha wagombea
wa ubunge katika Jimbo la Dimani, kwa upande wa udiwani katika Halmashauri 20
ni 13. Hivyo jumla ya wagombea wa nafasi ya udiwani ni 72,” alisema.
Jaji Kaijage alisema hadi sasa
pingamizi zilizokatwa ni sita na tano zimekatwa katika Kata ya Ihumwa, Manispaa
ya Dodoma na moja katika Kata ya Isagehe- Kahama.
Katika hatua nyingine, Jaji
Kaijage alisema atafanya kazi yake ya kuiongoza NEC kwa kuzingatia weledi na
kiapo chake alichoapa pamoja na sheria na kanuni.
Uchaguzi huo wa marudio
unafanyika kutokana na sababu mbalimbali, ikiwamo vifo, huku ule wa Dimani
unafanyika kutokana na kifo cha aliyekuwa Mbunge wake, Hafidh Ali Tahir (CCM),
kilichotokea Novemba 11, mwaka huu mkoani Dodoma, alikokuwa akihudhuria Mkutano
wa Bunge baada ya kuugua ghafla.
No comments