Breaking News

SERIKALI YATOLEA UFAFANUZI SAKATA LA TAARIFA ZA KUKAMATWA KWA WATANZANIA WANAODAIWA NI MAJASUSI NCHINI MALAWI



Baadhi ya Vyombo vya habari vya hapa nchini hivi karibuni vilitoa taarifa kuwa, Watanzania 8 wanaodaiwa kuwa ni majasusi wa Serikali ya Tanzania wamekamatwa nchini Malawi kwa tuhuma za kuingia kwenye mgodi wa urani wa Kayerekera uliopo nchini Malawi kinyume cha sheria.

Taarifa hiyo kwa mara ya kwanza ilitolewa na chombo cha habari cha Malawi ambacho kilidai kuwa watu hao wametumwa na Serikali ya Tanzania ili kuchunguza kama Serikali ya Malawi inatengeneza silaha za nyuklia kwa kutumia madini ya urani ya kutoka mgodi huo.

Kufuatia taarifa hizo, Wizara kupitia Ubalozi wa Tanzania nchini Malawi ulifuatilia ili kubaini ukweli wa tukio hilo. Baada ya kufuatilia ilibainika kuwa ni kweli Watanzania 8 kutoka taasisi ya CARTAS iliyo chini ya Kanisa Katoliki Songea mkoani Ruvuma walikamatwa na vyombo vya usalama katika Wilaya ya Karonga ambayo inapakana na Wilaya ya Kyela.

Watanzania hao mara moja walifunguliwa kesi kwa kutuhumiwa kufanya kosa la jinai la kuingia eneo la mgodi bila kibali (criminal trespass).

Ubalozi uliwasiliana na Taasisi ya CARTAS kutaka kufahamu madhumuni ya watu hao kufanya ziara nchini Malawi. Ubalozi ulielezwa kuwa ziara hiyo ilikuwa ni ya mafunzo ambapo walitaka kufahamu juu ya madhara yatokanayo na machimbo ya madini ya urani. Watanzania hao kwa sasa wapo katika gereza kuu la Mzuzu hadi kesi yao itakapotajwa tena tarehe 04 Januari 2017.

Ubalozi unaendelea kufanya mawasiliano na Kanisa Katoliki Songea ili kupata maelezo zaidi kuhusu ziara ya watu hao kwa madhumuni ya kuyawasilisha mamlaka husika ili watuhumiwa waweze kutolewa.

Aidha, Wizara kupitia Ubalozi umebaini kuwa CARTAS iliruhusu watu hao kufanya ziara nchini Malawi bila kupata kibali kutoka mamlaka husika na bila kutoa taarifa Ofisi ya Ubalozi kuhusu ziara hiyo.

Aidha, kipindi cha kufanya ziara hiyo nchini Malawi hakikuwa muafaka kwa kuwa watumishi wa Serikali ya Malawi wanakuwa katika likizo ya mwaka kuanzia tarehe 22 Desemba hadi 03 Januari 2017. Hii inakwamisha juhudi za kuwafuatilia watu hao ikiwa ni pamoja na kukwama kwa maombi ya kibali cha kuwatembelea watu hao tarehe 28 Desemba 2016.

Wizara inatoa wito kwa mara nyingine kwa taasisi za dini, vyuo vya elimu na watu binafsi kuomba vibali na kufuata sheria za nchi nyingine wanapofanya ziara za mafunzo au ziara nyinginezo ikiwa ni pamoja na kuwasiliana na ofisi za Balozi zetu kwa madhumuni ya kufahamishwa taratibu zinazotakiwa kufuatwa kabla ya kufanya ziara husika ili kuepuka usumbufu unaoweza kujitokeza.

Wizara, kupitia Ubalozi wa Tanzania nchini Malawi unaendelea na jitihada za kuhakikisha kuwa suala hilo linapatiwa ufumbuzi kwa haraka.

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki

Dar es Salaam, 29 Desemba  2016.

No comments