SAKATA LA KUCHOMWA MOTO MASHINE ZA KUVUTA MAJI WILAYANI KARATU WATU 12 PAMOJA NA VIONGOZI WA CHADEMA WASHIKILIWA NA POLISI ARUSHA
JESHI
la Polisi Mkoa wa Arusha linawashikilia watu 12, wakiwemo viongozi wa Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Mkoa wa Arusha.
Viongozi
hao walikamatwa kwa amri ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo wakituhumiwa
kuhusika kuchoma moto mashine za kuvuta maji kutoka kwenye chanzo cha Kangdet
wilayani Karatu kwa madai kwamba wanatekeleza agizo la Serikali, hatua ambayo
imeelezwa kuwa haikufuata utaratibu.
Akizungumza
na waandishi wa habari jana mjini Arusha, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha,
Charles Mkumbo, aliwataja waliokamatwa kuwa ni pamoja na Mwenyekiti wa Chadema
Wilaya ya Karatu, Moshi Darabe ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Barai,
anayedaiwa kuhamasisha wananchi kuchoma moto mashine hizo zenye thamani ya
zaidi ya Sh milioni 16.
Wengine
waliokamatwa ni Diwani wa Kata ya Mang’ola, Lazaro Emanuel, viongozi wa vijiji
vya kata hizo pamoja na baadhi ya wananchi.
Kamanda
Mkumbo alisema kuwa msako wa kuwakamata watuhumiwa wengine waliohusika na tukio
hilo bado unaendelea na uchunguzi utakapokamilika watafikishwa mahakamani kwa
hatua za kisheria.
Desemba
27, mwaka huu, kundi la wananchi wa vijiji vinne vya kata hizo waliandamana,
wakang’oa na kuchoma moto mashine za kuvuta maji katika chanzo cha maji cha
Kangdet, kinachotegemewa na vijiji vingine vya Kata ya Barai.
Kutokana
na tukio hilo, Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa ikiongozwa na mwenyekiti
wake ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Gambo, walitembelea eneo la tukio na
baada ya viongozi kueleza kilichotokea, aliagiza kukamatwa kwa watu wote
waliohusika na uharibifu huo.
“Sheria
lazima ichukue mkondo wake kwani agizo la Waziri Mkuu Kassim Majaliwa lilikuwa
wazi na halikusema wananchi wachukue sheria mkononi, jambo hili ni kinyume cha
sheria,” alisema Gambo katika mkutano huo.
Mwenyekiti
wa Halmashauri ya Wilaya ya Karatu, Jubilate Mnyenye (Chadema), amesema kuwa
yeye, mbunge wa jimbo hilo, Willy Qambalo na Mwenyekiti wa Kijiji cha Mang’ola,
Jacob Pius, wametakiwa kuripoti Kituo Kikuu cha Polisi jijini Arusha leo
asubuhi kwa mahojiano kuhusu tukio hilo.
No comments