TAARIFA YA UFAFANUZI KUHUSU MWANDISHI WA HABARI KUFIKISHWA MAHAKAMANI KWA AGIZO LA DC KAHAMA
Mkuu wa wilaya ya Kahama Fadhili Nkurlu,waandishi wa habari na baadhi ya wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama wilaya ya Kahama wakiwa katika kikao cha usuluhishi
Waandishi wa habari wakiwa katika ofisi ya mkuu wa wilaya ya Kahama
Kikao kinaendelea
Waandishi wa habari wakiondoka katika ofisi ya mkuu wa wilaya baada ya kikao kumalizika
TAARIFA
KWA UMMA
UONGOZI wa Klabu ya Waandishi
wa Habari mkoa wa Shinyanga (SPC),na baadhi ya waandishi wa habari wilayani
Kahama,wamekutana na mkuu wa wilaya ya Kahama Fadhili Nkurlu ili kupata muafaka
wa tatizo la kukamatwa na kufikishwa mahakamani mwandishi wa habari wa
kujitegemea Paul Kayanda.
Kikao hicho cha usuluhishi
kilichofanyika leo Jumamosi Desemba 31,2016 katika ofisi ya mkuu wa wilaya
hiyo,kimehudhuriwa pia na baadhi ya wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama wa
wilaya ya Kahama.
Kayanda alikamatwa jana Desemba
30,2016 na kufikishwa mahakamani kwa agizo la Mkuu wa wilaya ya Kahama Fadhili
Nkurlu akimtuhumu kuandika habari za kumdhalilisha na kuzisambaza kwenye barua
pepe mbalimbali za vyombo vya habari.
Katika kikao ,Uongozi wa Klabu
ya waandishi wa habari mkoa wa Shinyanga ,ulimuomba mkuu wa wilaya Nkurlu
kutaka kufahamu kilichomsukuma kuchukua maamuzi hayo,na nini ushauri wake juu
ya suala hilo lakini pia kumsikiliza mwandishi Paul Kayanda.
Baada ya kusikiliza pande zote
mbili,kikao kilibaini kuwepo kwa mapungufu katika habari iliyoandikwa na
Kayanda kuhusu habari ya laptop mbili zilizoibiwa nyumbani kwa mkuu huyo wa
wilaya.
Mkuu huyo wa wilaya alikiri
kuwepo kwa tukio la wizi nyumbani kwake lakini mwandishi huyo aliandika habari
kwa kuingilia uhuru binafsi wa kiongozi huyo akielezea watu wanaoingia na
kutoka nyumbani kwake lakini maisha anayoishi na kijana wake.
Kwa kuangalia maslahi mapana ya
umma kutokana na kutegemeana katika kusukuma maendeleo ya jamii baina ya
uongozi wa serikali na waandishi wa habari ,kikao kimemtaka Kayanda kumwomba
radhi mkuu huyo wa wilaya kwa kuingilia uhuru wake binafsi na kuuhusisha na
habari ya wizi wa laptop badala ya kujikita kwenye tukio la wizi wa laptop
pekee.
Kikao pia kimebaini kuwa pamoja
na mapungufu ya mwandishi, ni ukweli ulio wazi kuwa mkuu huyo wa wilaya
aliibiwa kompyuta mpakato (lap top) mbili nyumbani kwake na kuagiza vijana
watatu wakamatwe kwa mahojiano polisi akiwemo mmoja anayeishi nyumbani kwake japo
ameelezea kuwa hakujua walishikiliwa kwa siku ngapi.
Mkuu huyo wa wilaya pia
alieleza kukerwa na ujumbe mfupi wa maandishi kwa njia simu ya mkononi (sms)
alizodai kutumiwa na Kayanda kwa kutumia simu nyingine (tofauti na anayotumia)
zenye lugha ya kumtuhumu na kumdhalilisha.
Hata hivyo kikao hakikuona
kuwepo kwa ushahidi wa moja kwa moja kuthibitisha kama ni za mwandishi huyo
kweli au la huku kikao kikiomba sms hizo zifuatiliwe ili wamiliki wa namba hizo
wajulikane .
Baada ya kujadiliana kwa kina
katika kikao hicho kilichodumu kwa muda wa saa mbili,Kayanda amemwomba mkuu wa
wilaya msamaha kwa mapungufu yaliyojitokeza katika habari hiyo aliyoiandika, na
mkuu wa wilaya ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama wilaya ya
Kahama amekubali kumsamehe mwandishi huyo akiahidi kufuata taratibu zingine
kuondoa kesi mahakamani na kutaka kusafishwa katika mitandao mbalimbali ya
kijamii ilikoandikwa habari hiyo.
Nkurlu amesema anatambua kazi
nzuri inayofanywa na waandishi wa habari wilaya ya Kahama na mkoa wa Shinyanga
kwa ujumla katika kuandika habari zinazohusu serikali na akaomba kudumishwa kwa
ushirikiano uliopo baina ya viongozi wa serikali na waandishi wa habari ili
kusaidia kuharakisha maendeleo ya wananchi huku akiwasisitiza waandishi wa
habari kuzingatia weledi katika kazi zao.
Aidha Klabu ya waandishi wa
habari mkoa wa Shinyanga imewasisitiza waandishi wa habari kuzingatia weledi na
kufuata maadili katika kutekeleza majukumu yao ili kuepuka migongano isiyokuwa
na tija kwa umma.
Pia tunawashauri wadau wote wa
habari pindi inapotokea kuingia katika mgogoro wowote ama na waandishi wa
habari au chombo cha habari si vyema kwenda mahakamani moja kwa moja bali
wawasiliane na viongozi wa klabu za waandishi wa habari katika mkoa husika ili
kusuluhishana na kuwekana sawa.
Imetolewa na
Kadama Malunde
MWENYEKITI –SPC
No comments