RUFAA YA KESI LA MBUNGE LEMA SASA KUSIKILIZWA JAJI MAGIMBI
JAJI Salma Magimbi wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha ndiye
atakayesikiliza rufaa ya kutaka dhamana ya Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless
Lema, Desemba 28 mwaka huu katika Mahakama Kuu Kanda ya Arusha.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Wakili wa Lema,
Sheck Mfinanga alisema rufaa hiyo namba 126 ya mwaka 2016, imepangiwa
kusikilizwa na Jaji huyo. Alisema kimsingi wanalalamikia uamuzi wa Mahakama
kutomwachia huru, licha ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha kumpatia dhamana.
Awali, uamuzi uliotolewa Novemba 11 mwaka huu katika
Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha na Hakimu Desderi Kamugisha, ambapo Lema
anakabiliwa na kesi namba 440 na 441 za uchochezi dhidi ya Rais John Magufuli,
uliweka wazi dhamana.
Hakimu Kamugisha alikubali kutoa dhamana kwa madai kuwa
sheria haizuii kumpa dhamana mtu kwa kesi ya uchochezi, ila kabla ya kutoa
masharti ya dhamana licha ya kutamka dhamana ipo wazi, mawakili wa serikali
walipinga kumpatia dhamana Lema, kwa madai wameonesha nia ya kukata rufaa.
Kutokana na mawakili hao kusema hivyo, Hakimu aliamua kesi
hiyo ibaki kama ilivyo na mtuhumiwa asubiri maamuzi ya Mahakama Kuu.
Lema alilazimika kwenda mahabusu hadi sasa katika Gereza Kuu
la Kisongo. Baada ya hatua hiyo, mawakili wa Lema wakiongozwa na Sheck
Mfinanga, walianza kutafuta suluhisho la mteja wao kupata dhamana na walianza
na kuandika maombi na kuitaka Mahakama Kuu kufanya marejeo kwa kuitisha faili
la kesi hiyo kutoka Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha.
Lakini, ombi lilitupwa na Kaimu Jaji Mfawidhi, Sekela Moshi,
Novemba 11 mwaka huu kwa madai kuwa walikosea, badala ya kufanya marejeo
walitakiwa kukata rufaa. Mawakili hao walilazimika kukata rufaa siku hiyo hiyo
na Desemba 2 mwaka huu, ilitupwa na Jaji Fatuma Masengi kwa madai kuwa ilikuwa
nje ya muda.
Baada ya hatua hiyo, mawakili hao walipeleka ombi Mahakama
Kuu, kuomba kuongezewa muda wa kupeleka notisi ya kukata rufaa yao juu ya
dhamana na hatimaye Desemba 20, Jaji Dk Modesta Opiyo, alikubali na kumwongezea
muda Lema wa siku 10.
Siku hiyo ya kuongezewa muda, mawakili wa Lema walifanikiwa
kukata rufaa hiyo. Lema anashikiliwa kwa zaidi ya mwezi katika mahabusu ya Gereza
Kuu Kisongo.
Alikamatwa Novemba 2 mwaka huu nje ya viwanja vya Bunge
mjini Dodoma na alifikishwa mahakamani Novemba nane mwaka huu, akikabiliwa na
mashitaka ya uchochezi dhidi ya Rais John Magufuli.
|
No comments