MHE SAMIA SULUHU: SERIKALI YAJIPANGA KUREKEBISHA SERA NA SHERIA ZA KODI.
Makamo wa Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama Samia Suluhu akisoma hotuba wakati wa
uzinduzi wa mkutamo wa Chama cha Wasindikaji wa Vyakula nchini (TAFOPA)
uliofanyika jana katika ukumbi wa Mwl. Nyerere uliopo Jijini Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa Chama cha Wasindikaji wa Vyakula
nchini (TAFOPA), Susan Laizer akisoma hotuba ya chama hicho iliyoelezea
changamoto zinazowapata wajasiliamali hao katika shughuli za uzalishaji na
uuzaji wa bidhaa zao.Mkutano huo umefanyika jana katika ukumbi wa Mwl. Nyerere
uliopo Jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya
wajasiliamali wa Chama cha Wasindikaji wa Vyakula nchini (TAFOPA) wakisikiliza
kwa makini mafunzo yanayptolewa katika mkutano huo uliofanyika jana kwenye
ukumbi wa Mwl. Nyerere uliopo Jijini Dar es Salaam.
Na
Jacquiline Mrisho – MAELEZO.
Serikali
ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imejipanga kurekebisha Sera na Sheria za
kodi ili kuwasaidia wafanyabiashara na wajasiliamali kupata thamani ya shughuli
wanazozifanya.
Makamo
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama Samia Suluhu ametoa kauli hiyo
jijini Dar es Salaam alipokuwa akizindua Mkutano wa Chama cha Wasindikaji wa
Vyakula nchini (TAFOPA) uliofanyika katika ukumbi wa Mwl. Nyerere uliopo Jijini
humo.
Mama
Samia amesema kuwa wafanyabiashara na wajasiliamali nchini wamekuwa
wakilalamikia ongezeko la kodi katika bidhaa mbalimbali wanazozizalisha hadi
kupelekea kushindwa kuona faida ya shughuli hizo hivyo ni muhimu kwa Serikali
kusikiliza kilio chao kwa kutafuta namna bora itakayomaliza tatizo hilo.
“Serikali
ya Awamu ya Tano imeliona tatizo hilo na imeahidi kulifanyia kazi kwa kuzipitia
upya sheria hizo na kuzifanyia marekebisho ili kila mwananchi atoe kodi bila
kinyongo na apate faida ya shughuli anayoifanya,”alisema Mama Samia.
Amezitaja
changamoto zingine ambazo Serikali itazifanyia kazi ni kujenga miundombinu
katika maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya wajasiliamali, kupunguza muda wa
upatikanaji wa leseni za biashara pamoja na kuhakikisha Mamlaka ya Serikali za
Mitaa inatenga maeneo kwa ajili ya wajasiliamali hao.
Kwa
upande wake Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage amesema
kuwa jambo analojivunia katika uongozi wake ni kuweza kuwahamasisha Watanzania
kuelewa ujenzi wa uchumi wa viwanda ambapo kwa sasa nchi nzima wanazungumzia
habari hiyo.
“Asilimia
kubwa ya wananchi wanazungumzia namna ya kuanzisha viwanda kama sehemu ya
kujipatia kipato na ndio maana mikutano ya wajasiliamali imekua ikiongezeka
siku hadi siku, hii inaonyesha dhahiri kuwa watanzania wameamua kushirikiana na
Serikali katika kuinua uchumi wa nchi kupitia viwanda,”alisema Mwijage.
Naye
Mwenyekiti wa Chama cha TAFOPA, Susan Laizer amefafanua kuwa maeneo
yatakapotengwa yatasaidia kupunguza uharibifu wa mazao ya chakula yanayovunwa
wakati wa msimu husika pia yatatoa ajira nyingi kwa wananchi watakaokuwa
wakifanya shughuli za uzalishaji katika maeneo hayo.
“Tunaiomba
Serikali yetu itusaidie kutenga maeneo kwa ajili ya shughuli zetu hadi kwenye
sehemu za vijiji ili wakulima wapate soko la bidhaa zao kwa urahisi pamoja na
kuepuka madalali wanaozorotesha vipato vyao,”alisema Bi. Susan.
Aidha,
Bi Susan amempongeza Mama Samia kwa kuteuliwa na Umoja wa Mataifa kuwa mjumbe
wa nchi za Mashariki na Kusini mwa Afrika kwenye jopo la kuwawezesha wanawake
kiuchumi kwani ni sifa kwa Taifa na fursa kwa wasindikaji wote nchini.
Chama
hicho kimeanzishwa rasmi mwaka 1977 baada ya wanawake kupata mafunzo ya
usindikaji wa vyakula yaliyotolewa na Shirika la Maendeleo ya Viwanda Vidogo
Tanzania (SIDO) ikishirikiana na Shirika la Maendeleo ya Viwanda Vidogo Duniani
(UNIDO).
No comments