MECHI YA SIMBA NA YANGA IKO PALEPALE TFF YASEMA
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limesema kuwa mechi ya
ligi kuu Tanzania Bara ya mzunguko wa pili kati ya Simba na Yanga iliyokuwa
imepangwa kuchezwa Februari 18 mwaka 2017 iko palepale kwa kuwa bado
halijafikiria kuibadili tarehe hiyo.
Hatua hiyo inatokana na tarehe hiyo kugongana na kalenda ya
CAF ya michuano ya Klabu Bingwa Barani Afrika iliyotolewa hivi karibuni na
kuipanga Yanga kucheza mchezo wa marudiano kati yake na Ngaya de Mbe ya Comoro
kati ya tarehe 17, 18 na 19 mwezi Februari 2017.
Afisa Habari wa TFF Alfred Lucas amesema kuwa hadi sasa
shirikisho hilo kupitia Bodi ya Ligi halijafikiria kufanya mabadiliko yoyote
kwenye ratiba hiyo, na kwamba ratiba itaendelea kubaki kama ilivyo hadi hapo
itakapotangazwa vinginevyo.
"Ratiba imeshapangwa na haitabadilika, kila timu inajua
itacheza lini, kuhusu ratiba ya CAF haiwezi kutuzuia kufanya mashindano yetu,
kama kuna timu inacheza CAF inatakiwa ijipange, kila timu inatakiwa kuwa tayari
wakati wowote ndiyo maana zinafanya matayarisho, zinaajiri makocha, zinasajili
wachezaji , hiyo yote ni matayarisho kwahiyo sidhani kama watahitaji kupumzika
na kutuharibia ratiba" Amesema Lucas
Jumatatu iliyopita Mtendaji Mkuu wa Bodi ya ligi Boniface
Wambura akiwa kwenye kipindi cha 5Sports cha EATV, alisisitiza kuwa katika
mzunguko wa pili wa ligi, ratiba haitakuwa tatizo, na kwamba haitabadilishwa
badilishwa kwa kuwa katika upangaji wake kila kitu kilizingatiwa ikiwemo
kalenda ya CAF.
|
No comments