Breaking News

MCHUNGAJI LUSEKELO, (MZEE WA UPAKO) AFUKUZA WAANDISHI WA HABARI KANISANI



MCHUNGAJI wa Kanisa la Maombezi (GRC) la Ubungo jijini Dar es Salaam, Anthony Lusekelo maarufu 'Mzee wa Upako, aliwagomea waandishi wa habari kusikiliza hotuba yake ya ibada na kutuma wasaidizi wake wawaondoe waandishi hao.

“Samahani tunaomba muondoke kwani Mchungaji amesema hataki kumuona mwandishi hivyo tunaomba muende kwenye makanisa mengine,” alisema msaidizi huyo na kuhakikisha waandishi wote wanaondoka eneo hilo majira ya saa sita kasoro mchana.

Lusekelo maarufu Mzee wa Upako hivi karibuni amekuwa akirushiana maneno na baadhi ya waandishi wa habari baada ya kuandikwa akituhumiwa kuwa mlevi na kutukana hadharani.

Desemba 25 ya kila mwaka, waumini wa dini ya Kikristo nchini huungana na wenzao duniani kuadhimisha sherehe za kuzaliwa kwa Bwana wao Yesu Kristo yapata miaka 2000 iliyopita.

Wakati huohuo waumini wa dini ya Kikristo nchini wametakiwa kudumisha upendo, utii na unyenyekevu ili kuadhimisha kumbukumbu ya kuzaliwa kwa Bwana na Mwokozi wao Yesu Kristo ikiwa ni pamoja na kuliombea amani taifa lao la Tanzania.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kumaliza ibada ya mkesha wa sikukuu hiyo, Dk Alex Malasusa, Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Mashariki na Pwani, aliwataka waumini wa kanisa hilo, kuhakikisha wanakuwa mabalozi wa amani na upendo kwa wenzao.

Alisema siku ya Krismasi ni kumbukumbu ya kuzaliwa kwa mwana wa Mungu Yesu Kristo ambaye kutokana na upendo wake, aliwaunganisha watu na Mwenyezi Mungu.

“Tuuenzi upendo wake, lakini kubwa zaidi tukumbuke kuwa amani ndio msingi wa sikukuu hii. Hata alipokuja Yesu maneno yake ya kwanza yalikuwa ni amani,” alisisitiza. Askofu Malasusa, aliwataka wananchi katika kudumisha upendo huo, waliombee taifa pamoja na viongozi wake ili amani iliyopo iendelee kudumu.



Chanzo-Habarileo

No comments