Breaking News

MAPYA YAIBUKA KATIKA MSIBA WA ALIYEKUFA BAADA YA KUUMWA NA NYOKA WAKE, FAMILIA YADAI MZOGA WA NYOKA NA KUUZIKA NAE..HAKUNA NDUGU ALIYELIA




Frank Wandiba Jr



TUKIO la kushangaza lililohusishwa na kifo cha Denis Komba (24) baada ya nyoka aliyekuwa naye kuuawa, limechukua sura mpya baada ya mambo kadhaa kuibuka.

Hayo ni pamoja na familia kudai mzoga wa nyoka na kwenda nao kuuzika nyumbani, jambo lililoendelea kuhusisha suala hilo na imani za kishirikina.

Imeelezwa kuwa familia ilielezwa na mganga wa kienyeji kuwa mwili uliohifadhiwa hospitali, si wa mtoto wao, jambo lililowafanya kuuchukua mzoga wa nyoka na kwenda kuuweka katika mfuko wa sarandusi (kiroba) na kuuzika.

Hata hivyo, mashuhuda walieleza kuwa, familia hiyo ilikikata kichwa cha nyoka na kukizika kivyake na kiwiliwili sehemu nyingine huku mwili wa Komba ambaye naye alizikwa jana, ukizikwa katika kaburi eneo lingine tofauti. Tukio hilo ni la juzi na lilimhusu Komba, mkazi wa Mateka, manispaa ya Songea mkoani Ruvuma.

Nyumbani kwao ni kilometa tano kutoka katikati ya mji wa Songea. Kabla ya maziko, baadhi ya vijana waliokuwa wamebeba jeneza, walikuwa wakikimbia nalo mwendo wa mchakamchaka huku wakiimba “mkimbize mkimbize nyoka awahi asije kudhuru watu wengine”.

 
Katika maziko hayo, hakuna ndugu aliyeonekana kulia wala hakukuwa na ibada yoyote wakati jina la marehemu linadhihirisha kuwa ni wa imani ya Kikristo. Wakati hayo yakiendelea msibani, baadhi ya watu wake wa karibu walidai alikuwa na tabia ya kucheza na nyoka mara kwa mara.

Hata hivyo, baba mzazi alikana kumuona mwanawe na nyoka. Naye daktari aliyechunguza mwili, alisema kifo cha Komba kinatokana na kugongwa na nyoka mwenye sumu kali, lakini hakuna jeraha wala alama yoyote iliyoonekana katika mwili huo.

Familia yachukua mzoga wa nyoka

Habari zinaeleza kuwa juzi familia ilikwenda kuzungumza na watu wa Idara ya Maliasili, waliochukua mzoga wa nyoka kwa uchunguzi kama nyara ya serikali. Walikubaliana kuwa familia itakwenda kuufukia na ndipo Maliasili walimrudisha nyoka hadi eneo la tukio na familia kumchukua.

Ilielezwa kuwa hatua hiyo, inatokana na madai kuwa kuna mganga amehusisha mzoga wa nyoka huyo na mwili wa Komba.

Watu wa karibu wa familia hiyo, ambao hawakutaka kutaja majina yao gazetini wakiwemo mafundi seremala na majirani, walieleza kuwa familia wakiongozwa na baba mzazi Sevelin Komba, walirudi eneo la tukio baada ya kutoka kwa mganga wa kienyeji na kumchukua nyoka na kumpeleka nyumbani.

Habari zinaeleza kuwa familia baada ya tukio hilo, walikwenda kwa mtaalamu wa mambo ya asili (mganga wa kienyeji) ambaye hakufahamika mara moja na kuelezwa kwa nini wamekubali kumuacha mtoto wao akiteseka juani kwani mwili walioupeleka nyumbani kutoka hospitali si wa Denis (Komba).

Aidha familia baada ya kumchukua nyoka huyo eneo la tukio alikouawa, baada ya kufikishwa nyumbani alikatwa kichwa kwa makubaliano ya familia ya marehemu na kiwiliwili kuzikwa tofauti na kichwa katika mfuko wa sarandusi. Baba mzazi alikanusha suala hilo la kwenda kwa mganga.

Katika maziko hayo, hakukuwa na chakula wala matanga na watu wengi walijitokeza ili kushuhudia kitakachoendelea. Alizoea kutembea,kucheza na nyoka Kwa mujibu wa majirani hao ni kwamba kwa muda mrefu Komba alikuwa na vitendo vinavyoashiria mambo ya kishirikina.

Kwamba hata huyo nyoka, si mara yake ya kwanza kutembea naye, kwani alikuwa akionekana naye mara kwa mara hasa katika viwanja vya mpira, kwa kuwa marehemu alikuwa mpenzi mkubwa wa mchezo wa mpira wa miguu.

Walisema Komba (Denis) alikuwa na vitendo vya kishirikina na alifahamika sana kwa jina ‘Dogo Mzimu’, kutokana na kuwa na mambo makubwa ya yakishirikina tofauti na umri wake, jambo lililosababisha hata baadhi ya watu wengine mtaani kwake kumuogopa licha ya upole wake.

Baba mzazi azungumza

Baba mzazi wa Komba, Sevelin Komba akizungumzia maisha ya mtoto wake kabla ya tukio hilo, alisema ni mtoto wa kwanza kati ya watoto watano na kwa muda wote wa maisha yake alikuwa kijana mzuri, ambaye alikuwa anajishughulisha na kazi ya useremala, ujenzi wa nyumba pamoja na kilimo.

Alisema, wiki tatu zilizopita yeye na familia yake akiwemo Denis walikwenda shamba katika kijiji cha Mpitimbi Songea vijijini kwa ajili ya shughuli za kilimo kwani ni kawaida ya familia hiyo kila inapofika msimu wa kilimo wanakwenda kulima kwa ajili ya kupata chakula cha familia.

Lakini baada ya wiki moja, yeye kama kiongozi wa familia, alirudi nyumbani kwa ajili ya kufanya maandalizi ya kupata mahitaji ikiwemo chakula na vitu mbalimbali pindi wanapoendelea na shughuli zao za kilimo na kuwaacha watoto wake wakiongozwa na Denis shambani.

Alisema hata hivyo, siku mbili kabla ya tukio hilo tarehe 25, Denis alirudi nyumbani kutoka kijijini kwa ajili ya kufuata mahitaji, ambayo baba yake tayari alishanunua na siku iliyofuata tarehe 26 asubuhi Denis alipewa mahitaji yote muhimu na kurudi shambani huku akiwa na baiskeli.

Hata hivyo, siku hiyo ya tarehe 26 majira ya saa 4 usiku, alipigiwa simu na watu waliojitambulisha kwamba ni wauguzi katika hospitali ya mkoa Ruvuma na kumtaarifu kwamba mtoto wake, Denis, yupo hospitali amepata matatizo hivyo anahitajika kufika haraka.

Komba alisema, mara baada ya kufika hospitali ya mkoa, alishangaa kuona kuna umati mkubwa wa watu wakiwemo askari polisi na waendesha boda boda, ambapo alielezwa kuhusu tukio la kifo cha Denis na alioneshwa mwili wa marehemu mtoto wake, lakini alishangaa kumuona mtoto wake Denis mwili ukiwa na tope.

Komba (baba) alieleza kuwa, wakati huo wote hakuambiwa chanzo cha kifo cha mwanawe hadi siku ya pili ambayo alipata taarifa kuwa kifo cha mtoto wake, kimesababishwa na kufa kwa nyoka aliyekuwa akimmiliki, ambaye alipigwa na wananchi kufuatia kutaka kugonga mwendesha boda boda.

Alisema, ilipofika siku ya pili majira ya mchana, alichukuliwa hadi kituo kikuu cha polisi mjini Songea na baadaye kupelekwa idara ya Maliasili, nje ya mji wa Songea na kuoneshwa nyoka aliyemgonga mtoto wake , ambaye bado alikuwa chini ya ulinzi wa maofisa maliasili Kanda ya Kusini.

Kwa mujibu wa baba huyo, jana saa 1 usiku baada ya kikao cha familia kilichofanyika mchana, walikubaliana waende eneo la tukio baada ya maofisa maliasili kumrudisha nyoka huyo akiwa ameshakufa hadi eneo hilo. Ndipo familia walipomchukua na kumpeleka nyumbani kwa Denis, ambaye katika uhai wake alikuwa na mke na mtoto mmoja.

Alisema, wakiwa katika maandalizi ya mazishi ya Denis baadhi ya majirani waliofika nyumbani kwa ajili ya kushiriki maandalizi ya mazishi, walitaka Denis azikwe kaburi moja na nyoka wake, jambo ambalo familia wamekataa, kwa kuwa yule ni binadamu na nyoka ni mnyama, ambaye ni adui kwa binadamu.

Baba amkata kichwa nyoka Hata hivyo, jambo la kushangaza baba wa marehemu amemkata kichwa nyoka na kusisitiza kwamba Denis atazikwa pekee yake, kiwiliwili cha nyoka kitazikwa peke yake na kichwa kifukiwe eneo lingine, kitendo kinachoaminika ni jambo la kishirikina.

Mafundi seremala, bodaboda wanena

Wakizungumza na gazeti hili kwa masharti ya kutotajwa majina yao baadhi ya mafundi seremala, ambao marehemu Denis alifanya nao kazi kwa karibu walisema kuwa, Denis licha ya kuonesha vitendo vingi vilivyoashiria mambo ya kishirikina, lakini alikuwa kijana mpole na mwenye upendo mkubwa kwa wenzake.

Lakini, walisema hawaamini kama kifo cha Denis, kimetokana na kuumwa na nyoka, bali kimetokana na mambo ya kishirikina yaliyopelekea yeye kupoteza maisha kwa vile nyoka huyo alikuwa akimuongoza katika mambo mbalimbali.

“Sisi tunakuambia hivi huyu alikuwa anamtumia sana nyoka kwa imani za kishirikina kwani alikuwa naye mara kwa mara hata akiwa katika matembezi ya kawaida na alimtumia katika shughuli zake,”walisema.

Daktari azungumzia uchunguzi

Kwa mujibu wa daktari aliyemfanyia uchunguzi Denis, Dk Geofrey Mdede alisema kifo cha Denis kimetokana na kugongwa na nyoka mwenye sumu kali.

“Kwa utaratibu wa hospitali mgonjwa akishafariki kama ni kifo cha mashaka huwa tunamfanyia uchunguzi ili kubaini chanzo chake na tulipomfanyia Denis tukabaini amekufa baada ya kugongwa na nyoka,” alisema Dk Mdede.

“Lakini kwa bahati mbaya sana sikuona eneo aliloumwa na nyoka kwani meno ya nyoka ni madogo sana kama sindano na laiti marehemu angekuwa hai basi angeonesha eneo alilogongwa na nawaomba sana jamii iamini kwamba kifo cha Denis kimetokana na kugongwa na nyoka,”alisema.

Denis azikwa

Denis amezikwa jana katika makaburi ya Mateka huku umati mkubwa wa watu ukifurika kwa ajili ya kushuhudia na kushiriki maziko yake. Vijana waliobeba jeneza waliimba nyimbo mbalimbali na kulikimbiza jeneza kwa mtindo wa mchakamchaka wakisema mkimbize mkimbize nyoka awahi asije kudhuru watu wengine.

Dereva wa bodaboda aathirika kisaikolojia

Habari zilizopatikana ni kwamba dereva wa boda boda, Kassian Haule ambaye baada ya tukio hilo alilazwa katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Ruvuma kwa ajili ya uchunguzi zaidi, jana ameruhusiwa kutoka hospitali hapo.

Hata hivyo, kwa mujibu wa madereva wenzake wa bodaboda, Haule ameanza kupoteza kumbukumbu ya mambo mbalimbali.

Maliasili wamzungumzia aina ya nyoka huyo

Mhifadhi wa Wanyamapori wa Hifadhi ya Taifa ya Selous Kanda ya Kusini, Msondi Simwanza, alisema aina ya nyoka aliyehusika katika tukio hilo ni ‘blackmamba’ na ni kati ya nyoka hatari duniani kwa sumu kali.

Simwanza alisema nyoka wa aina hiyo, hupenda kuishi kwenye mazingira yenye vichaka, hasa kwenye mashimo ya vichuguu au mengineyo. Juzi, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma, Zuberi Mwombeji alithibitisha tukio hilo. Alisema mwili wa marehemu haukuwa na jeraha lolote.

Alisema nyoka aliyeuawa na wananchi alichukuliwa na idara ya mali ya asili. Pia alisema uchunguzi wa tukio hilo unaendelea ili kubaini kiini cha tukio hilo la kuuawa kwa nyoka na kisha mmiliki wake naye kufa.

NA MUHIDIN AMRI- SONGEA

No comments