MAJAMBAZI YAVAMIA MGODI NA KUUA WATU WAWILI
WATU wawili wamekufa huku wengine wanne wakijeruhiwa baada
ya majambazi walio na silaha kuvamia mgodi wa dhahabu wa Nholi uliopo wilaya ya
Bahi mkoani Dodoma.
Majambazi hao wanadaiwa kupora dhahabu, fedha na mali
nyingine na kuwavua watu nguo na kuondoka nazo.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk Charles Kiologwe alikiri
kupokelewa kwa miili ya watu wawili hospitalini hapo na majeruhi wanne.
Alisema mwili mmoja upo katika hali mbaya. Waliofariki dunia
katika tukio hilo, walitajwa kuwa ni Lukumale Membo na mwingine aliyefahamika
kwa jina moja la Hamisi.
Kwa mujibu wa Muuguzi Msaidizi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa
wa Dodoma, Melisiana Danford, maiti hao na majeruhi walipokelewa hospitalini
hapo saa 6 usiku kuamkia jana mara tu baada ya kutokea kwa tukio hilo. Majeruhi
katika tukio hilo ni Sunday Undi (49), Lawrence Mhagama (35) , Maila Mchele
(44) na Sophia Sayuni (37).
Wakizungumza katika wodi namba moja ambako wamelazwa,
majeruhi hao walisema walivamiwa na majambazi, ambao baadaye waliwapiga risasi
na kusababisha vifo vya watu wawili na wengine kujeruhiwa.
Lawrence Mhagama ambaye amepigwa risasi mguu wa kushoto,
alisema amekuwa akiendesha shughuli za uchimbaji mdogo kwenye mgodi huo.
Alisema siku ya tukio majira ya saa mbili usiku akiwa ndani, alisikia milio ya
risasi nje na alipojaribu kutoka, alipigwa risasi ambayo ilimjeruhi mguuni.
“Chanzo cha tukio kwa kweli sikijui ila majambazi
walituvamia , mimi ni mgeni eneo hilo nilikwenda kwa ajili ya kazi ya mgodi,
nimepigwa risasi mguuni ambapo mpaka sasa bado ninayo mwilini, wanasema
wataniruhusu nikipata nafuu na baadaye wataangalia uwezekano wa kuitoa risasi
hiyo,” alisema.
Alisema majambazi hao, walipora mali nyingi ambapo waliwavua
watu nguo na kuondoka nazo huku wakiacha watu uchi.
Majeruhi mwingine aliyelazwa wodi namba moja, Sunday Undi,
alisema walivamiwa na majambazi hao majira ya saa mbili kasorobo usiku wa
kuamkia juzi, wakiwa kwenye kioski cha Maila Mchele, wakipata vinywaji na
kuendelea na mazungumzo.
“Tulivamiwa tukasikia tunaambiwa tuko chini ya ulinzi, kwa
vile lilikuwa ni tukio la kushtukiza tukawa tunashangaa, wakapiga risasi juu
ikabidi tuingie ndani ya kibanda kile baada ya muda tukajikuta watu saba tukiwa
chini ya kitanda,” alisema.
Alisema majambazi hao waliwaamrisha watoke na kuwaambia kila
mtu atoe alichonacho na aliyekuwa akikataa, aliamriwa kuvua nguo.
“Walininyang’anya fedha na simu, wakatuvua na suruali
wakaondoka nazo, mimi binafsi wamenipora Shilingi milioni mbili nilizokuwa
nazo,” alisema.
Alisema majambazi hao walikuwa zaidi ya wanne na walikuwa
wamevalia kininja. Alisema mtu aliyejaribu kuwatazama usoni, alikuwa akipigwa
risasi. Majeruhi mwingine katika tukio hilo, Maila Mchele ambaye amelazwa wodi
hiyo akiwa hajitambui, amejeruhiwa vibaya.
Inadaiwa alipigwa risasi tumboni na kutokea upande wa pili.
Majeruhi wa nne, Sophia Sayuni (37) amelazwa wodi namba 10 hospitalini hapo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Lazaro Mambosasa
alipohojiwa kuhusu tukio hilo, alisema atalitolea ufafanuzi baadaye.
|
No comments