PICHA: RAIS MAGUFULI NA MKEWE WALIVYOSHIRIKI IBADA YA KRISMASI MKOANI SINGIDA
Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli na Mkewe Mhe. Mama Janeth
Magufuli, leo tarehe 25 Desemba, 2016 wameungana na waumini wa Jimbo Katoliki
la Singida kusali Misa ya Krismasi iliyofanyika katika Kanisa Kuu la Moyo
Mtakatatifu wa Yesu Mjini Singida.Misa hiyo Takatifu ya Krismasi imeongozwa na
Askofu wa Jimbo Katoliki la Singida Mhashamu Edward Mapunda.
Akizungumza mara baada
ya kumalizika kwa Misa Takatifu, Mhe. Rais Magufuli amewatakia heri ya Krismasi
waumini wote wa Jimbo la Singida na Watanzania wote kwa ujumla na amewasihi
kusherehekea kuzaliwa kwa Bwana Yesu kwa kuendeleza amani na upendo na kuacha
vitendo vya kubaguana kwa misingi ya dini, kabila, itikadi na kanda zao.
Dkt. Magufuli
amewahimiza Watanzania wote kuongeza juhudi katika kuchapa kazi kama
alivyofanya Bwana Yesu na pia amesema kwa kuwa maeneo mengi ya nchi yameonekana
kukabiliwa na uhaba wa mvua, ni vema wakatumia vizuri mvua chache zinazoendelea
kunyesha kuzalisha mazao yanayokomaa haraka ili kuepuka upungufu wa chakula.
Kwa upande wa Mkoa wa
Singida ambao ni maarufu kwa kilimo cha alizeti, Mhe. Rais Magufuli
amewasisitiza kuchangamkia fursa ya ujenzi wa viwanda ambayo nchi inatoa
kipaumbele kwa kuzalisha alizeti kwa wingi ili zitumike kuzalisha mafuta ya
kupikia kwa wingi.
Jaffar Haniu
Naibu Mkurugenzi wa
Mawasiliano ya Rais, IKULU
Singida
25 Desemba, 2016
|
No comments