TWAWEZA - ASILIMIA 95 YA WATANZANIA WANAPENDA SERIKALI IKOSOLEWE,ASILIMIA 29 WAPO TAYARI KUANDAMANA
Asilimia 95 ya wananchi wanathamini uwezo wa kuikosoa serikali
Na wananchi 7 kati ya 10 wanasema demokrasia ndiyo mfumo bora wa utawala
Na wananchi 7 kati ya 10 wanasema demokrasia ndiyo mfumo bora wa utawala
29 Septemba 2016, Dar es Salaam: Demokrasia na uhuru wa kutoa maoni ni vitu viwili vinavyothaminiwa sana na wananchi.
Asilimia 95 ya wananchi wanauthamini uwezo wa kuikosoa serikali pale wanapoona imekosea.
Na asilimia 69 wanakubali kuwa demokrasia ni mfumo bora wa utawala japokuwa baadhi ya wananchi wanasema kwa kiwango fulani, utawala usio wa kidemokrasia unaweza kukubalika.
Hata hivyo asilimia kubwa ya wananchi (asilimia 86) wanasema kuwa Tanzania inahitaji vyama vingi vya siasa ili kuwapa wananchi fursa ya kumchagua kiongozi anayewafaa kuwaongoza.
Matokeo haya yametolewa na Twaweza kwenye muhtasari wake uitwaoDemokrasia, udikteta na maandamano: Wananchi wanasemaje?Muhtasari huu unatokana na takwimu kutoka Sauti za Wananchi, utafiti wa kwanza barani Afrika wenye uwakilishi wa kitaifa unaotumia simu za mikononi.
Matokeo haya yanatokana na takwimu zilizokusanywa kutoka kwa wahojiwa 1,602 kati ya tarehe 23 na 29 Agosti mwaka 2016. Utafiti huu unahusisha Tanzania bara tu. (Zanzibar haihusiki kwenye matokeo haya)
Pamoja na kukubalika kwa serikali ya kidemokrasia, wananchi wana maoni tofauti tofauti kuhusu majukumu ya vyama vya upinzani.
Asilimia 80 wanasema baada ya uchaguzi, vyama vya upinzani vikubali kushindwa na visaidiane na serikali kuijenga nchi.
Ni asilimia 20 tu wanaosema wapinzani waifuatilie na kuiwajibisha serikali iliyopo madarakani.
Vilevile, asilimia 49 wanasema mikutano baada ya kipindi cha kampeni hukwamisha maendeleo lakini asilimia 47 wanasema vyama vya upinzani viruhusiwe kufanya mikutano yao bila pingamizi.
Huu tena ni mgawanyiko miongoni mwa wafuasi wa vyama: asilimia 71 ya wale wanaoshikamana na vyama vya upinzani wanaunga mkono kufanyika kwa mikutano ukilinganisha na asilimia 37 ya wafuasi wa chama tawala.
Pamoja na hayo, asilimia 60 ya wananchi wanakubaliana na kuzuiwa kwa mikutano ya vyama vya siasa ikihusisha asilimia 70 ya wafuasi wa chama tawala na asilimia 33 ya wafuasi wa vyama vya upinzani. Kwa upande wa ushiriki kwenye maandamano, asilimia 50 hawapo tayari, japokuwa asilimia 29 wapo tayari kuandamana.
Wananchi wanaoshikamana na vyama vya upinzani wapo tayari zaidi kushiriki kwenye maandamano (43 asilimia ukilinganisha na asilimia 27 ya wafuasi wa chama tawala) na vijana wanaonekana kuwa tayari zaidi kushiriki kwenye maandamano (asilimia 35 ya vijana wenye umri wa miaka 18-29, tofauti na asilimia 15 ya wananchi wenye umri wa miaka zaidi ya 50).
Ndani ya miezi michache baada ya kuanzishwa kwake, harakati za UKUTA zimefahamika na asilimia 16 ya wananchi.
Kati yao, asilimia 48 wanaeleza kuwa ni Umoja wa Kupinga Udikteta na asilimia 22 wanaunga mkono UKUTA.
Asilimia 55 ya walio karibu na vyama vya upinzani wanaunga mkono harakati za UKUTA huku asilimia 44 wakiwa hawaungi mkono.
Idadi ndogo (asilimia 6) ya wafuasi wa chama tawala wanaunga mkono juhudi za UKUTA.
Mwananchi mmoja kati ya kumi anafahamu kuhusu UKUTA na anasema alipanga kushiriki kwenye maandamano. Mingoni mwani ni asilimia 3 ya wafuasi wa chama tawala na asilimia 24 wa upinzani.
Kwa ujumla, asilimia 11 wanaamini Tanzania inaoongozwa na dikteta, huku asilimia 58 wakipinga. Makundi mbali mbali katika jamii yametoa maoni tofauti kuhusu suala hili, ikiwa wafuatayo, wakikubali kuwa udikteta upo nchini:
- Wanaume: asilimia 13 | wanawake: asilimia 8
- Wenye umri kati ya 18 – 29: asilimia 13 | wenye umri zaidi ya miaka 50: asilimia 4
- Matajiri: asilimia 16 | masikini: asilimia 8
- Waliosoma: asilimia 26 | ambao hawajasoma: asilimia 4
- Wafuasi wa vyama vya upinzani: asilimia 29 | wafuasi wa chama tawala: asilimia 5
“Utafiti huu umeibua matokeo ya kufikirisha juu ya mitazamo ya Watanzania kuhusu siasa na mfumo wa utawala,” anasema Mkurugenzi Mtendaji wa Twaweza, Aidan Eyakuze, “Watanzania wengi sana wanauunga mkono mfumo wa demokrasia ya vyama vingi na uhuru wa kukusanyika na kutoa maoni. Hili ni jambo la kuzingatiwa na serikali. Kwa sasa, idadi kubwa ya wananchi hawakubaliani na kauli inayosema kuwa Rais Magufuli ni dikteta. Inaonekana kwamba wananchi wanasema ili kulinda amani na kuchochea kasi kubwa zaidi ya maendeleo wanaweza kukubaliana na baadhi ya vizuizi kwenye haki za binadamu. Lakini iwapo vitendo visivyo vya kidemokrasia vitavuka mipaka, utayari wao wa kuvikubali unaweza ukabadilika.”
No comments