Breaking News

CHADEMA IRINGA YASAIDIA ZAIDI YA WANAFUNZI MIA MBILI (200) KUENDELEA NA MASOMO

1
 Diwani wa  viti maalum CHADEMA Sara Mwajeka na  Mwalimu mkuu wa shule ya msingi Igumbilo, Fredrick Asenga wakionyesha mfano wa sare za wanafunzi walizotoa msaada

 Naibu Meya wa manispaa ya Iringa Joseph Lyata na Mwalimu mkuu wa shule ya msingi Igumbilo, Fredrick Asenga wakiwa tayari kukabidhi sare kwa wanafunzi
  Hawa ni baadhi ya wanafunzi mia mbili (200) wanaoishi katika mazingira magumu wanatarajiwa kusaidiwa msaada wa pesa kwa ajili ya kununulia sabuni,nauli kila wiki na sare za shule ya msingi.


                                                              NA FREDY MGUNDA,Iringa

ZAIDI ya wanafunzi mia mbili (200) wanaoishi katika mazingira magumu wanatarajiwa kusaidiwa msaada wa pesa kwa ajili ya kununulia sabuni na nauli kila wiki na wanawake walionda timu maalum ya kutoa msaada kutoka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).


Msaada huo unatarajiwa kutolewa kwa wanafunzi wanaoishi katika mazingira magumu kutoka kata nne zilizoko manispaa ya Iringa ambazo ni Miyomboni, Igumbilo, Kitanzani na Ruaha na kugharimu zaidi ya shilingi milioni 3.5


Akizungumza wakati wa kuwakabidhi msaada wa sare za shule,viatu na soksi wanafunzi hao, katika hafla fupi ya iliyofanyika katika shule ya msingi ya Igumbulo, Diwani wa   viti maalum CHADEMA Sara Mwajeka alisema kuwa wameamua kuwasaidia wanafunzi hao kwa lengo la kuwapatia elimu bora japo kuwa misaada hiyo haiwezi kumaliza shida zao.


Mwajeka aliongeza kuwa wanafunzi wenye mazingira magumu wanatakiwa kusoma ili taifa lipate wasomi wengi wenye tija ya kuisaidai nchi yao kuendelea kiuchumi.

“Mimi kama mama napata uchungu kuona wanafunzi wenye mazingira magumu wanasoma kwa taabu huku wana uwezo mkubwa darasani,hivyo tunajitaidi na kujikuna pale tunapoweza kuwasaidia wanafunzi nawaomba watu wenye uwezo kuwasaidia wanafunzi wote wenye mazingira magumu” alisema Mwajeka.


Kwa upande wake Naibu Meya wa manispaa ya Iringa Joseph Lyata aliwapongeza timu ya wanawake wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) manispaa ya Iringa kwa kutoa msaada huo ambao ni mkubwa kwa maisha ya wanafunzi wanaoishi kwenye mazingira magumu.


“Tanzania yetu kuna matajiri wengi sana lakini wanashindwa kuwasaidia watoto wanaoishi katika mazingira magumu lakini wakimama hawa wamejitoa kwa kile walicho nacho kuwasaidia wanafunzi hao hivyo nami naunga mkono kuendelea kuchangia watoto hawa” alisema Lyata


Aidha Lyata aliwataka viongozi wa nchi kuwaangalia wanafunzi wanaoishi katika mazingira magumu ili kufuata na kumuenzi Mwalimu Nyerere kwa vitendo kwani alikuwa anapenda sana elimu ili wananchi waweze kuongeza ufahamu na kujua mbinu za kujitegemea na sio kuomba omba kila siku.


“Jamani kusaidia wanafunzi wenye mazingira magumu hawana idikadi ya vyama,dini wala makabila tunatakiwa kuwasaidia kutokana na uwezo wetu wa kifedha,mm nimekuwa mwalimu kwa muda mrefu na nayajua matatizo ya wanafunzi wenye mazingira  wanavyosoma kwa taabu ni aibu kwa taifa kama Tanzania kuwa wanafunzi wanaoteseka kama hawa” alisema Lyata.


Naye Mwalimu mkuu wa shule ya msingi Igumbilo, Fredrick Asenga aliwashukuru timu ya wanawake wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na Naibu Meya, Joseph Lyata kuwa kuwasaidia wanafunzi wa shule hiyo kwani wamewapunguzia na kuwaondolea aibu iliyokuwa inawakumba kutokana na umasikini wao.


“Wanafunzi hawa walikuwa wanavaa sare ambazo zilikuwa zimechanika na ilikuwa aibu kwa wanafunzi wengine lakini kwa msaada huu mmefanya wajisikie nao ni matajiri na najua sasa watasoma kwa bidii bila kujiangalia  wamekaaje hongereni sana na karibuni tena kuendelea kuwasaidia wanafunzi hawa” alisema Asenga.

Misaada hiyo imetolewa na timu ya wanawake wa chama cha demokrasia na maendeleo(CHADEMA) manispaa ya Iringa kwa lengo la kuwasaidia watoto wenye mazingira magumu wasome wakiwa na furaha kwa kuwa nao ni binadamu kama binadamu wengine.

No comments