WAKINAMAMA DAKAWA WAFUGA NYUKI KUPAMBANA NA UHARIBIFU WA MAZINGIRA
TAKRIBAN
kilometa 10 kutoka Kijiji cha Dakawa kuna kitongoji cha Magogo
kilichoko msituni kabisa ambako pia kuna mashamba ya mpunga.
Msitu
huu ambao bado ungali na miti mingi ya asili ambayo imenusurika
kucharangwa na wachoma mkaa na wanaotafuta ardhi yenye rutuba kwa ajili
ya kilimo, ndiko akinamama wapatao 30 wameamua kutundika mizinga kwa
ajili ya ufugaji wa nyuki katika shamba lenye ukubwa wa ekari nne.
Licha ya
kujikwatua vilivyo, lakini wanapoingia katika msitu huu akinamama hawa
hawana mchezo kabisa, baadhi yao wanavaa mavazi maalum ya kujikinga na
nyuki na kuanza kukagua mizinga yao kama tayari nyuki wamekwishaingia.
Ofisa Nyuki
wa Wilaya ya Mvomero, Oscar Kunambi (aliyechuchumaa kushoto) akisaidiana
na mwanakikundi cha Dakawa Green Voices, Neema Obeid, kuweka vizuri
mzinga.
“Kujipamba
ni jambo la kawaida, lakini tunapokuja huku tuko kikazi zaidi,” anasema
Neema Obeid huku akipenya kwenye vichaka kuiendea mizinga ambayo iko juu
ya miti mikubwa.
Akina mama
hao wa kikundi cha Dakawa Green Voices Women Group wameamua kuingia
kwenye ujasiriamali wa ufugaji wa nyuki kwa malengo makubwa mawili –
kupata fedha kutokana na mazao ya nyuki pamoja na kupambana na
mabadiliko ya tabinchi.
“Misitu
inateketea, watu wanaendelea kuchoma mkaa na wengine wanafyeka miti ili
wapate mashamba, lakini kwa kuanzisha ufugaji huu wa nyuki, kamwe
hatutakubali kuona yeyote akikata hata fimbo, achilia mbali miti
mikubwa,” anasema Bi. Mariam Bigambo, mshiriki kiongozi wa mradi huo.
Mwanahabari
Judica Losai (wa pili kushoto) akimuuliza maswali Ofisa Nyuki wa Wilaya
ya Mvomero, Oscar Kunambi, wakati wakiwa kwenye eneo la ufugaji wa
nyuki.
Mariam
Bigambo ni miongoni mwa akinamama 10 waliopatiwa mafunzo nchini Hispania
mapema mwaka huu na wanatekeleza kwa vitendo mradi wa Green Voices,
ambao unafadhiliwa na taasisi inayojihusisha na maendeleo ya wanawake wa
Afrika, ijulikanayo kama Women for Africa Foundation inayoongozwa na
Makamu wa Rais mstaafu wa Hispania, MarÃa Teresa Fernández de la Vega.
Hapa nchini, mradi huo unasimamiwa na asasi ya Environment Media Agenda
(EMA) chini ya uratibu wa Bi. Secelela Balisidya
Akinamama
wengine wanatekeleza miradi mbalimbali ya ujasiriamali unaoendana na
mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabianchi katika mikoa ya Dar es
Salaam, Morogoro, Kigoma, Kilimanjaro, Pwani na Mwanza.
Mama Bigambo
anasema kwamba, ufugaji huo unahitaji kutunza mazingira ili kuwawezesha
nyuki kupata chakula chao hasa nekta na maji, hivyo ni vizuri
kuhakikisha mazingira yanakuwa salama.
Baadhi ya mizinga ya akinamama wa Dakawa Green Voices ikionekana kuning’inia kwenye miti. Mizinga hii tayari ina nyuki.
Aidha,
anasema kwamba, kwa kuwa Tanzania, kama zilivyo nchi nyingine duniani,
inakabiliwa na mabadiliko ya tabianchi, ni vizuri kufanya shughuli za
uchumi zinazohakikisha kwamba mazingira yanatunzwa na wakati huo huo
shughuli hizo zikichangia kupambana na mabadiliko ya tabiachi, huku
ufugaji wa nyuki ukiwa miongoni mwa shughuli hizo.
“Bila
kutunza mazingira hata hao wanaokata mkaa na wanaotafuta mashamba
watalia baadaye kwa kuwa miti itakwisha, tutabaki na jangwa ambao
halitatoa mazao tena. Tutakufa,” anasisitiza.
Kuhusu
ufugaji huo wa nyuki, Mama Bigambo anasema kwamba, ingawa zamani
ilionekana kama shughuli za akina baba, lakini kama wanawake
watafundishwa wanaweza kuendesha ujasiriamali huo bila shida.
“Gharama
kubwa ya ufugaji wa nyuki iko mwanzoni tu – kutafuta mizinga pamoja na
eneo bora linalofaa kwa ufugaji ambalo maua na maji yanapatikana kwa
urahisi, baada ya hapo kazi yako ni kutembelea na kuangalia maendeleo.
Akinamama wa Dakawa Green Voices wakisikiliza maelezo kutoka kwa mtaalam wa ufugaji nyuki, Oscar Kunambi, ambaye hayupo pichani.
“Nyuki
hawachungwi kama ng’ombe, mbuzi au nguruwe wala hawaangaliwi kama kuku,
hawahitaji chanjo ya ugonjwa wowote, hivyo ni rahisi kutundika mizinga
yako katika eneo husika na kuendelea na shughuli zako nyingine,”
anafafanua.
Akizungumzia
umuhimu na faida za nyuki, Mama Bigambo anasema kuwa licha ya kusaidia
kutunza mazingira, lakini nyuki ni muhimu kwa maisha ya binadamu na
viumbe hai vyote, kwani ndio wanaofanya uchavushaji wa mimea.
Anazitaja faida za ufugaji nyuki kuwa ni asali na nta, mazao ambayo yana faida kubwa hata katika soko la kimataifa.
Ofisa nyuki wa Wilaya ya Mvomero,, Oscar Kunambi, akiwaelekeza akinamama wa Dakawa Green Voices namna ya ufugaji bora wa nyuki.
Katibu wa
kikundi hicho, Amina Buteta, ana matumaini makubwa kwenye mradi huo na
anasema kwamba unaweza kuwakomboa wanawake wa Dakawa na vijiji vya
jirani kwa kujipatia kipato kikubwa.
“Tunakuja
huku shamba kila baada ya wiki, wakati mwingine tunakuja kwa zamu
kuangalia maendeleo, hivyo hatubanwi na ufugaji wa nyuki na tunaendelea
na shughuli zetu nyingine,” anasema.
Amina
anasema kwamba, wameanza na mizinga 30, lakini malengo yao ni kuwa na
mizinga 4,000, lakini changamoto wanayokabiliana nayo ni mtaji wa
kununulia mizinga hiyo.
Inaelezwa
kwamba, mzinga mmoja unauzwa Shs. 70,000, lakini kutokana na uchumi kuwa
mdogo, wengi wanashindwa kupata fedha za kununulia.
“Lakini ipo siku tutafanikiwa tu, hakuna shida, kwa sababu tumedhamiria,” anasema.
Ofisa
Mtendaji wa Kijiji cha Dakawa, Andrea Muhando, anasema ufugaji wa nyuki
siyo tu utawakomboa kiuchumi wanawake hao na jamii nzima kwa ujumla,
lakini utasaidia kutunza mazingira katika eneo hilo ambalo limeshindwa
kuzalisha mazao vya kutosha kutokana na mafuriko ya mara kwa mara pamoja
na mvua zisizo za uhakika.
Anasema,
kukosekana kwa mvua katika misimu tarajiwa kama ilivyokuwa zamani pamoja
na mafuriko makubwa yanayosababisha maafa ni matokeo ya mabadiliko ya
tabianchi, hivyo ni vyema wananchi wakaangalia miradi mingine endelevu
yenye kipato lakini inayoweza kutunza mazingira.
“Kila mwaka
mvua zinashindwa kunyesha kwa wakati na kwa kiwango kinachotakiwa, na
zinaponyesha zinakuja kwa nguvu na kuleta madhara hata kwa mimea kama
tunavyoshuhudia katika eneo hili kila mwaka.
“Mwaka huu
mafuriko yameharibu hekta 240 za mazao mbalimbali, ukiwemo mpunga ambao
umekuwa mkombozi wa mkulima, na sasa tunategemea tu katika maeneo ya
kondeni pekee,” anasema.
Kwa upande
mwingine, Ofisa Nyuki wa Wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro, Oscar
Kunambi, anasema kwamba kuanzishwa kwa mradi wa akinamama hao
kutachochea jamii kuingia kwenye ufugaji wa nyuki wilayani humo badala
ya kutegemea kilimo na mifugo pekee.
Anasema
kwamba, soko la asali ni kubwa nchini Tanzania, ambapo tayari kuna
kiwanda kikubwa wilayani Kibaha kinachohitaji malighafi lakini asali
inayozalishwa haitoshelezi mahitaji.
Aidha,
anasema kwamba, wilaya hiyo ina maeneo mengi yenye misitu ambayo
ikitumiwa kwa ufugaji wa nyuki inaweza kuleta faida kubwa kwa jamii na
taifa kwa ujumla.
“Unapofuga
nyuki, mbali ya kupata faida kutokana na mazao yake, lakini unasaidia
kuyalinda maeneo hayo kwa sababu hakuna mtu mwenye akili timamu
anayeweza kwenda kukata miti sehemu ambayo kuna nyuki, kwanza usalama
wake utakuwa mdogo,” anasema.
Vyanzo vya habari vinaeleza kwamba, asali ina soko zuri kwani kilo moja inauzwa kwa Shs. 15,000 ikiwa shambani.
Kwa mujibu
wa Kunambi, mzinga mkubwa wa kisasa una uwezo wa kutoa kati ya kilo 10
hadi 20 za asali baada ya miezi sita tangu nyuki kuingia kwenye mzinga.
Amewataka
wananchi katika wilaya hiyo kujitokeza na kuanzisha miradi ya ufugaji
nyuki, huku akiahidi kwamba yuko tayari kufanya kazi usiku na mchana
kuwasaidia utaalamu na ushauri.
Mkurugenzi
wa Wilaya ya Mvomero, George Mkindo, amewapongeza akinamama hao kwa
jitihada zao na akasema halmashauri yake itawaunga mkono kwa kila hali.
“Nimeambiwa
kwamba wanahitaji shamba, nadhani itakuwa vyema kama tukiongea na vijiji
ili kutenga mashamba kwa ajili ya ufugaji wa nyuki kwa sababu
inatupunguzia hata sisi kazi kubwa ya kupambana na waharibifu wa
mazingira, kwa kuwa wananchi wenyewe watakuwa walinzi,” anasema.
No comments