ALEX MSAMA: AMWANGUKIA MWAKYEMBE, ASEMA “NAKUOMBA RADHI”
Bw
. Alex Msama akizungumza na waandishi wa habari wakati alipomuomba
Radhi Mh. Dk. Harisson Mwakyembe Waziri wa Sheria na Katiba kutokana na
Gazeti la Dira analomiliki kumuandika vibaya.
………………………………………………………………………………………………………..
MFANYABIASHARA Alex Msama
amemuomba radhi Waziri wa Sheria na Katiba, Dk. Harrison Mwakyembe
kufuatia habari mbili zilizochapishwa katika Gazeti la Dira ya Mtanzania
analolimiliki.
Akizungumza leo na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Msama alisema amejiridhisha kuwa habari hiyo iliyobeba kichwa cha habari ‘Utapeli wa Mwakyembe wamwagwa hadharani’ haikufuata misingi ya uandishi wa habari.
Akizungumza leo na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Msama alisema amejiridhisha kuwa habari hiyo iliyobeba kichwa cha habari ‘Utapeli wa Mwakyembe wamwagwa hadharani’ haikufuata misingi ya uandishi wa habari.
Habari nyingine ambayo imeonekana
kumchafua Dk Mwakyembe ni ile ya Mwakyembe atuhumiwa kutapeli bilioni 2
ambazo zimemuumiza kiongozi huyo.
Alisema yeye kama mmiliki wa
gazeti hilo amesikitishwa na habari hiyo na kwamba hatua ya kwanza
anayoichukua ni kumuomba radhi Waziri Mwakyembe.
Msama alisema sambamba na kuomba radhi atamfikishia barua Mwakyembe ya kumtaka radhi kwa tukio hilo.
“Nimesikitishwa na habari hii kwa
kuwa haikuzingatia misingi ya uandishi wa habari, ilihukumu na
kuonyesha kuwa lengo lake lilikuwa kumharibia jina Waziri Mwakyembe,
ninachukua nafasi hii kumuomba radhi nikiwa mmiliki wa gazeti hilo,”
alisema Msama.
Aidha Msama alisema hatua
nyingine anayochukua ni kumsimamisha kazi mhariri wa gazeti hilo, Mussa
Mkama kwa kuwa alishindwa kufanya kazi yake kwa umakini ya kuhakikisha
habari anazozipitisha zinafuata misingi ya uandishi wa habari na weledi.
Alisema Mkama alipaswa
kuhakikisha anafuata weledi lakini alishindwa kufanya hivyo kwa hiyo
anamsimamisha kazi na kwamba hatua nyingine kali za kinidhamu zitafuata.
“Mimi ni mfanyabiashara sijui
mambo ya uandishi, nilimuajiri nikiamini atasimamia yale aliyofundishwa
chuoni, kwa kuwa ameshindwa inabidi akae pembeni kwanza,” alisisitiza
Msama.
Ameahidi kuwa katika Gazeti la Dira ya Mtanzania litakalotoka Juni 27, kwa ukubwa uleule atamuomba radhi Waziri Mwakyembe.
Hivi karibuni Waziri Mwakyembe
aliitisha mkutano wa waandishi wa habari mjini Dodoma akilalamikia kuwa
habari mbili za gazeti hilo iliyochapishwa na Gazeti la Dira ya
Mtanzania la Juni 20 na la Juni 23 mwaka huu zililenga kumchafua na
kuahidi kuwa atalishtaki kupitia habari hizo mbili.
No comments