Breaking News

WAZIRI KOMBO ASHIRIKI HAFLA YA KUMBUKUMBU YA SIKU YA KUZALIWA MFALME WA JAPAN

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb.) ameshiriki katika hafla ya kusheherekea miaka 65 ya kuzaliwa Mtukufu Naruhito, Mfalme wa Japan iliyofanyika katika makazi ya Balozi-Mteule wa Japan hapa nchini jijini Dar es Salaam. 

Wakati wa hafla hiyo, Mheshimiwa waziri Kombo amepongeza uhusiano mzuri wa kidiplomasia wa miaka 64 uliopo kati ya Tanzania na Japan. 

Vilevile, amepongeza mchango wa Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Japan (JICA) tangu mwaka 1962 katika kuunga mkono jitihada za serikali hususan katika sekta za nishati, kilimo, maji, miundombinu, kujengeana uwezo n.k. 
Sanjali na hilo aliishukuru Serikali ya Japan kupitia JICA kwa kutekeleza miradi mbalimbali hapa nchini ikiwemo Mfugale flyover, Daraja la Gerezani, Daraja la Salenda na soko la samaki la Malindi lililopo Zanzibar. 

Halikadhalika, Mheshimiwa Waziri Kombo aliipongeza ushirikiano wa miaka 32 wa Afrika na Japan kupitia Mkutano wa Kimataifa wa Tokyo kuhusu Maendeleo ya Afrika (TICAD) ulioanzishwa mwaka 1993. Mheshimiwa Waziri Kombo alisisitizia kuwa Mkutano wa TICAD umeunga mkono jitihada za Afrika katika kuimarisha biashara na uwekezaji na kuhakikisha maendeleo endelevu kwa nchi za Afrika. 
 
Kwa upande wake Mhe. Yoichi Mikami, Balozi-Mteule wa Japan nchini Tanzania alielezea kufurahishwa na ushirikiano wa Tanzania na Japan na muingiliano mzuri wa watu.

Sanjali na hilo, Balozi-Mteule Mikami alisisitizia dhamira ya Japan ya kuzidi kuimarisha ushirikiano huo wa uwili na kupitia mwamvuli wa TICAD.

No comments